NA JANETH MUSHI,-ARUSHA
MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe, amemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), ambaye bado yuko mahabusu katika Gereza la Kisongo mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana baada ya kuonana na mbunge huyo, Rungwe alisema baadhi ya matatizo yanayotokea kwenye jamii yanasababishwa na baadhi ya watawala.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiibua chuki miongoni mwa wananchi jambo ambalo si zuri na linahitaji kukemewa.
Kiongozi huyo alimtembelea Lema akiwa amefuatana na viongozi mbalimbali akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chauma, Kayumbo Kabutali na wabunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare na Moshi Vijijini, Antony Komu, wote wa Chadema
“Historia ya zamani inatufunza matatizo yanayotokea katika jamii yanachangiwa na mambo yanayotendwa na baadhi ya watawala ambayo yanaleta chuki.
“Na chuki siyo kitu kizuri kwa sababu inazidi kuwa kubwa kwenye mioyo ya watu hata kama wako kimya,”alisema na kuongeza:
“Hili limewahi kutokea enzi za mitume hata Nelson Mandela aliwekwa ndani na alipotoka dunia nzima iliamka hivyo tunaona kuna baadhi ya watu wanawekwa ndani bila sababu ya msingi, natoa wito kwa wenye mamlaka kuangalia suala hili.”
Mwenyekiti huyo alisema ni wakati wa watanzania wote kwa ujumla kupigia kelele suala hilo kwa vile Mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi, anazuiliwa kwa makosa yenye dhamana jambo la kukemewa.
“Tumekuja Arusha kumuangalia Lema kwa sababu ni mwenzetu na tuna masikitiko na kama walifikiri wakimuweka Lema ndani wanamsimamisha au kumkomesha, wanamkomaza kisiasa.
“Anapata ujasiri wa aina Fulani kwa sababu haelewi kwa nini yuko ndani, wangemkuta na malori matatu ya silaha sawa,” alisema.
Mbunge wa Bukoba Mjini alisema ameridhishwa na kupata matumaini na hali ya mbunge huyo kwa vile ni yuleyule na ameongeza ujasiri wa kulisema lile analoamini.
Naye Mbunge wa Moshi Vijiji, Antony Komu, alisema Lema ameomba wabunge wote bila kuangalia itikadi za vyama vyao wanapaswa kuwa makini wakati wa utungaji wa sheria.
Alisema kutokana na baadhi ya upungufu wa sheria kuna watu wako gerezani kwa muda mrefu.
Alisema katika gereza hilo asilimia kubwa wako gerezani kwa muda mrefu kutokana na upungufu wa sheria mbalimbali.