Na Kadama Malunde-Shinyanga
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limemtaka Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ajisalimilishe kwa kupeleka vibali kuondoa utata wa gari alilokuwa akilitumia katika kampeni za uchaguzi mdogo uliofanyika Januari 22, mwaka huu wilayani Kahama.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita, alisema kiongozi huyo anasakwa kutokana kuwapo taarifa za intelijensia zinazoeleza alikuwa akitumia gari hiyo ambayo haikuwa na vibali.
Mwita alisema jeshi hilo linamtaka Zitto apeleke taarifa kuhusu gari analomiliki aina ya Toyota Land Cruiser V8 ambalo hakulitaja namba za usajili.
“Siku ya kufunga mkutano wa kampeni uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Isagehe wilayani Kahama, tulipata taarifa kwamba Kabwe anatumia gari ambalo si halali, halina vibali.
“Tukawa tumefikiria tumpate baada ya mkutano atupe maelezo kuhusu gari analolimiliki, lakini kabla hata hatujaonana naye, alitoweka,” alisema Mwita.
Alisema Jeshi la Polisi linamtaka kiongozi huyo wa ACT Wazalendo apeleke vibali vya gari hilo.
“Kwa hiyo sisi mpaka sasa Kabwe tunamtaka atuletee vibali vya gari hilo na ndiyo kitu ambacho sisi tunamuhitaji.
“Baada ya kuona gari hilo linachukua muda mrefu kwetu tulimkabidhi dereva wa gari hilo na kumtaka amtafute bosi wake atuletee vibali vya gari hilo,” alisema.