WAANDISHI WETU DAR, IRINGA
KAULI za makamanda wa polisi, Lazaro Mambosasa wa Kanda Maalumu Dar es Salaam na Juma Bwire wa Iringa kuhusu kutoweka kwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo (24), zimezua utata baada ya kukinzana.
Wakati Kamanda Mambosasa akisema Nondo alikamatwa akiwa Mafinga akiendelea na shughuli zake, Kamanda Bwire alieleza awali kuwa mwanafunzi huyo aliripoti polisi Mafinga.
Machi 8, baada ya Nondo kupatikana, Kamanda Bwire alizungumza na waandishi wa habari akaeleza kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu, kitivo cha siasa na utalawa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye inasemekana alipotea katika mazingira ya kutatanisha mkoani Dar es Salaam.
“Jana tarehe saba, mwezi wa tatu, majira ya saa moja alifika katika Kituo cha Polisi cha Mafinga, |Wilaya ya Mufindi na kueleza kuwa ametekwa na watu wasiofahamika,” aikaririwa akieleza Kamanda Bwire.
Baada ya kuhojiwa mkoani Iringa, Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), alisafirishwa kuletwa Dar es Salaam.
Juzi, Kamanda Mambosasa alizungumza na waandishi wa habari akaeleza kuwa ili kuthibitisha kile kilichokuwa kimezagaa kuwa ametekwa na watu wasiojulikana, hakuripoti mahali popote, si kwa mwenyekiti wa mtaa, si kwa afisa mtendaji wa kata wala kituo chochote cha polisi mkoani Iringa, alikamatawa akiwa Mafinga akiendelea na shughuli zake za kawaida.
Wafafanua kauli zao
Kutokana na kauli hizo, gazeti hili liliwatafuta makamanda hao ili kufafanua kauli zao.
Kamanda Bwire alisema suala la Nondo kwa sasa linachunguzwa na Jeshi la Polisi, Dar es Salaam hivyo hawezi kulizungumzia.
Kwa upande wake Kamanda Mambosasa alisema kwa kawaida upelelezi hauwezi kuwekwa hadharani, bali kinachotolewa ni matokeo ya upelelezi huo.
“Hayo ni matokeo ya upelelezi kwa hiyo uchunguzi umeonyesha hivyo, tena ni uchunguzi wa kisayansi.
“Yani utekwe usinyang’anywe simu kisha uachiwe bila kuripoti popote uendelee na kazi zako,” alisema Kamanda Mambosasa.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.