MANCHESTER, ENGLAND
NAHODHA wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney, ameweka wazi kuwa mara baada ya kumalizika kwa msimu huu ataondoka ndani ya kikosi hicho na kujiunga na mchezo wa mieleka wa WWE.
Mchezaji huyo amedai kuwa mchezo wa mieleka ni miongoni mwa vitu ambavyo vilikuwa kwenye ndoto zake kwa kipindi kirefu, hivyo huu ni wakati wake sahihi wa kufanya maamuzi hayo.
Katika mashindano mbalimbali ya mieleka ya WWE, mchezaji huyo amekuwa akionekana mara kwa mara. Hata hivyo, leo hii anatarajia kukutana na bodi ya mchezo huo.
Mchezaji huyo msimu huu amekuwa akikosa namba mara kwa mara ndani ya kikosi cha Man United chini ya kocha wao Jose Mourinho na alihusishwa kutaka kukimbilia katika ligi ya nchini China na Marekani.
Klabu mbalimbali za nchini China zilikuwa tayari kuweka mezani kitita cha pauni milioni 52 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 142, lakini hadi usajili wa Januari mwaka huu unakamilika mchezaji huyo hakuweza kuondoka Man United, lakini kwa sasa yupo tayari kuondoka na kujiunga na mchezo huo wa mieleka.
“Kutimkia kwenye mchezo wa mieleka wa WWE ni sehemu ya ndoto zangu ambazo nilikuwa naziota mara kwa mara tangu nikiwa na umri mdogo, nimekuwa nikivutiwa na nyota wa mchezo huo kama vile Dwayne Johnson ‘The Rock’ Stone Cold Steve Austin, lakini si Alan Shearer au David Seaman.
“Nimefanya mazungumzo na kocha wangu, Jose Mourinho, mara baada ya kiungo Bastian Schweinsteiger kutangaza kuondoka, lakini mazungumzo yetu hayakuwa mazuri hivyo ni lazima niondoke.
“Nilikuwa nahitaji changamoto mbalimbali, hivyo ninaamini kwenye mchezo huu wa WWE itakuwa ni sehemu yangu sahihi, nimefanya mazungumzo na Zlatan Ibrahimovic na amenishauri jinsi ya kwenda kutengeneza jina upya kama ilivyo kwa Lionel Messi na Paul Pogba,” alisema Rooney.
Rooney mwaka huu ametajwa kuwa mfungaji bora wa kipindi chote ndani ya kikosi cha Manchester United, hata hivyo amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha timu ya Taifa ya England kwa muda mrefu.