MKONGWE wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney, ameweka wazi kuwa kiungo wa Juventus ambaye anatarajia kujiunga na United, Paul Pogba, biashara yake haijakamilika.
Pogba ni mchezaji ambaye anasubiriwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka wa klabu ya Manchester United na wadau mbalimbali wa soka hasa kutokana na uhamisho wake kuwa wa fedha nyingi.
Mchezaji huyo anatarajia kuvunja rekodi ya usajili duniani kama atafanikiwa kujiunga na Mashetani hao Wekundu wa Jiji la Manchester wakiwa chini ya kocha wao mpya, Jose Mourinho
Rooney anaamini kuwa mchezaji huyo atajiunga na klabu hiyo katika kipindi hiki cha majira ya joto lakini biashara ya uhamisho wake hadi sasa haijakamilika.
“Ninamjua vizuri Pogba, ninatamani atue Old Trafford katika kipindi hiki cha usajili, amekuwa akionesha uwezo mkubwa tangu alipoondoka katika klabu hii miaka minne iliyopita.
“Hadi sasa uongozi wa klabu hii unaendelea na mipango ya kutaka mchezaji huyo arudi katika klabu yake ya zamani, ninaamini itawezekana japokuwa biashara bado haijakamilika.
“Kama atakuwa tayari kujiunga na klabu yetu basi na sisi tutakuwa na furaha kubwa kumuona mchezaji huyo akiungana nasi na tutampokea na kushirikiana naye kwa moyo mmoja kwa kuwa ni mchezaji bora kwa sasa katika ulimwengu wa soka,” alisema Rooney.
Hata hivyo, mchezaji huyo amemmwagia sifa mshambuliaji mpya wa klabu hiyo, Zlatan Ibrahimovic, ambaye tayari ameonesha cheche zake katika michuano ya kimataifa ya kirafiki ya Kombe la ICC.
“Kama Pogba atajiunga na sisi tutatengeneza timu bora ambayo itakuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa pamoja na waliosajiliwa msimu huu.
“Ujio wa Ibrahimovic kutoka klabu ya PSG umezidi kutuweka katika ubora mpya kwa kuwa mchezaji huyo ana uwezo mkubwa na ameonesha uwezo wake kwenye michuano ya ICC.
“Ameanza vizuri kama ilivyo kwa nyota ambao walisajiliwa msimu uliopita, Anthony Martial na Marcus Rashford, kwa sasa tupo katika ubora mzuri tunaamini tutaleta changamoto kubwa msimu huu katika Ligi Kuu na ikiwezekana tuchukue ubingwa,” aliongeza.
Usajili wa Pogba umekuwa gumzo kwenye mitandao mbalimbali, wiki iliyopita kuna taarifa zilisema kwamba tayari mchezaji huyo amefanyiwa vipimo na klabu hiyo nchini Marekani na ilisemekana kuwa amebakisha saa 48 kuweza kutua Old Trafford, lakini bado.