WANAMICHEZO wa michuano ya Olimpiki nchini Brazil, wameingia hofu ya ubora wa miundombinu mara baada ya juzi kuanguka kwa sehemu ya uwanja wa Marina da Gloria.
Uwanja huo ambao upo kando kando ya bahari umekutwa sehemu ya uwanja huo ukiwa umeanguka kutokana na kupigwa na wimbi kubwa la maji usiku wa kuamikia jana.
Kutokana na hali hiyo wanamichezo mbalimbali wamepata wasiwasi na ubora wa miundombinu hiyo kabla ya kuanza kwa michuano hiyo Ijumaa ya wiki hii.
Msemaji wa michuano hiyo, Philip Wilkinson, ameweka wazi tatizo lililosababisha sehemu ya uwanja huo kuanguka lakini hakuna majeruhi yoyote ambayo yametokea.
“Ni tatizo ambalo limetokea kutokana na wimbi kubwa la maji ambalo lilipiga kwenye kuta za uwanja huo, lakini tunashukuru hakuna mtu ambaye amepata majeruhi kutokana na tukio hilo.
“Kampuni ambayo ilihusika kujenga viwanja hivyo itahusika katika kufanya marekebisho kwa sehemu ambayo imeharibika, tunaamini kuna vipande vya chuma na taka taka mbalimbali zimeingia kwenye maji kutokana na kubomoka huko, hivyo ni vizuri watu wasiyatumie maji hayo kwa kuweka mdomoni kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.
“Lakini hakuna haja ya kulifanya jambo hili kuwa kubwa, ni tatizo la kawaida ambalo limetokea na tunawahakikishia kwamba kila kitu kutakuwa vizuri na salama wataalamu wanaendelea na ukarabati wa sehemu hiyo,” alisema Wilkinson.