LONDON, ENGLAND
NAHODHA wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Alan Shearer, amemtaka nahodha wa sasa katika timu hiyo, Wayne Rooney, kustaafu kuitumikia timu hiyo na nguvu zake azielekeze katika klabu yake.
Rooney mwenye umri wa miaka 30, ameitwa katika kikosi cha kocha mpya wa timu hiyo, Sam Allardyce, kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia ambao utapigwa dhidi ya Slovakia Jumapili mwishoni mwa wiki hii.
Nyota huyo amekuwa nahodha wa timu hiyo tangu 2014, katika michuano ya Kombe la Dunia, lakini katika michuano ya Kombe la Euro 2016 nchini Ufaransa, mchango wa mchezaji huyo ulikuwa mdogo.
Kutokana na hali hiyo, Shearer anaamini kuwa nguvu zilizobaki kwa mchezaji huyo ni kuitumikia klabu yake ya Manchester United na si timu ya taifa tena.
“Huu ni wakati wa Rooney kuwa mbinafsi na kuanza kujifikiria mwenyewe juu ya mchango wake kwa sasa katika timu ya taifa, naweza kusema kuwa ni wakati sahihi wa kusema inatosha kuitumikia timu ya Taifa.
“Sina maana kwamba uwezo wa mchezaji huyo umekwisha, ila ana umri wa miaka 30 kwa sasa pia ni nahodha wa klabu na timu ya taifa, hivyo ni ngumu kwa mchezaji huyo kutoa mchango sawa kwa pande zote mbili.
“Kwa upande wangu, nilistaafu soka huku nikiwa na umri wa miaka 29 ambapo ilikuwa mwaka 2000, lakini kikubwa ambacho kilinifanya kustaafu ni kutokana na kusumbuliwa na majeruhi. Kipindi hicho kuna baadhi ya watu walisema kuwa nina ubinafsi, lakini ukweli ni kwamba nilikuwa naijua afya yangu,” alisema Shearer.
Hata hivyo, nyota huyo wa zamani amedai kuwa Rooney akifanya hivyo ataweza kuitendea haki klabu yake ya Manchester City.
“Wakati ninaamua kuachana na timu ya taifa niliweza kutumia nguvu zangu kwa klabu ya Newcastle, hivyo Rooney akifanya hivyo ataweza kuonesha ubora wake kwa Manchester United,” aliongeza.
Rooney hadi sasa amecheza michezo 115 katika timu hiyo ya taifa na kufanikiwa kufunga mabao 53, huku mabao saba yakiwa ya mikwaju ya penalti.