31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ronaldo atwaa tuzo Real Madrid

MADRID, HISPANIA

NYOTA wa zamani wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, juzi alitwaa tuzo ya ‘Marca’ ikiwa ni kukumbukwa kwa mchango wake alioutoa kabla ya kuondoka na kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Italia, Juventus.

Tuzo hiyo ilianzishwa na gazeti la Marca mwaka 1997, ikiwa inatolewa kwa wanamichezo ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwa timu yao, hivyo Ronaldo amechukuwa kutokana na historia aliyoiacha ndani ya Santiago Bernabeu.

Ronaldo kwa sasa anaungana na wanamichezo mbalimbali waliowahi kuchukua tuzo hiyo kama vile Michael Jordan, Pele, Rafa Nadal, Novak Djokovic, Muhammad Ali, Usian Bolt, Michael Phelps, Michael Schumacher, Diego Maradona, Lionel Messi na wengine wengi.

Katika historia, Ronaldo amefanikiwa kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano, Kombe la Dunia kwa klabu mara nne, European Super Cups mara tatu, Ligi Kuu England mara tatu, La Liga mara mbili, Serie A mara moja, European Championship mara moja na UEFA Nations League. 

Ronaldo ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Juventus, juzi alikuwa jijini Madrid na kuhudhuria kwenye sherehe za tuzo hiyo huku akiwa na mke wake Georgina Rodriguez.

“Sehemu kubwa ya tuzo hii ni kutokana na kile nilichokifanya wakati nipo katika klabu ya Real Madrid, nawashukuru sana kwa sapoti kubwa niliyoipata hapa,” alisema Ronaldo.

Mchezaji huyo aliongeza kwa kuwaomba radhi mashabiki wa Madrid kwa kitendo cha kuondoka na kujiunga na Juventus mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2018.

“Ninaomba radhi kwa kuondoka Madrid, nimekuwa nikiyakumbuka maisha ya Manchester na Madrid, lakini kutokana na maisha naweza kusema nimekaa sana Madrid, watoto wangu na mke wangu wote wamezaliwa hapa, hivyo napakumbuka sana Madrid.

“Tuzo hii itakuwa sehemu muhimu ya kumbukumbu zangu, Madrid ni sehemu maalumu nimezunguka sana lakini ni miji michache kama Madrid, hivyo ninaamini nitarudi tena Madrid hivi karibuni,” aliongeza Ronaldo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles