27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ronaldo apania kumfikia Messi

Picha ya tatuZURICH, USWISI
NYOTA waReal Madrid, Cristiano Ronaldo, usiku wa kuamkia jana alifanikiwa kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia ‘Ballon d’Or’ kwa mara ya pili mfululizo, huku mwaka huu akipanga kuchukua tena na kumzidi nyota wa Barcelona, Lionel Messi aliyeitwaa mara nne.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Ureno aliwapiku wapinzani wake, Messi na kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer, waliokuwa wakishindanishwa kuwania tuzo hiyo.

Nyota hao watatu pia walifanikiwa kuorodheshwa kwenye kikosi bora cha mwaka jana cha Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), sambamba na wachezaji wengine mabeki Philipp Lahm, David Luiz, Thiago Silva na Sergio Ramos, viungo ni Andres Iniesta, Toni Kroos na Angel Di Maria pamoja na Arjen Robben, ambaye ni mshambuliaji.
Tuzo hiyo inamfanya Ronaldo, 29, kufikisha jumla ya tuzo tatu za Ballon d’Or na kuwafikia magwiji wa zamaniJohan Cruyff, Michel Platini na Marco van Basten waliotwaa idadi sawa kama yeye, huku akiwa na mtihani mzito wa kumfikia Messi anayeongoza kwa kutwaa mara nne.

Mara baada ya kutwaa tuzo hiyo Ronaldo alisema:”Nataka kuwa mchezaji mkubwa duniani wa muda wote na hii inahitaji jitihada kubwa, lakini nina imani ya kufika huko…Napenda kuwashukuru mashabiki wangu wote walionipigia kura na wachezaji wenzangu wa Madrid, rais wetu wa klabu na kocha wangu. Bila shaka ulikuwa mwaka wenye mafanikio sana kwetu.”

Naye Rais wa Real Madrid, Flolentino Perez, alifurahishwa na tuzo ya mchezaji wake huyo huku akieleza tayari nyota huyo ameshapanga kuitwaa tena mwaka huu na kumfikia mpinzani wake Messi.

“Cristiano anataka kuvunja kila rekodi,” alisema. “Anataka kuchukua tuzo ya nne ya Ballon d’Or na anafanya kazi ya kuishinda na ameanza vema mwaka huu, pia kama alivyosema, jambo la muhimu ni timu inacheza vizuri, ni timu kubwa La Liga, inafanya makubwa na kwa yote hayo inakuja tuzo ya mtu binafsi.”

Baada ya kumpata mshindi, FIFA ilitoa orodha ya wachezaji 10 walioingia 10 bora ya tuzo hiyo na asilimia za ushindi wao,Ronaldo (37.66%), Messi (15.76%), Neuer (15.72%), Robben (7.17%), Thomas Muller (5.42%), Lahm (2.90%),Neymar (2.21%), James Rodriguez (1.47%), Toni Kroos (1.43%), Angel Di Maria (1.29%).

Mbali na tuzo hiyo iliyoteka hisia za watu wengi, FIFA ilitoa nyingine ambazo ni;

Mchezaji bora wa kike

Kiungo wa klabu ya Wolfsburg na timu ya taifa ya Ujerumani ya wanawake, Nadine Kessler, alitwaa tuzo hiyo akimpiku nyota wa Brazil, Matra na nyota mwingine wa Marekani Abby Wambach.

“Moyo wangu unagonga mapigo ya ajabu wakati huu, sikuwahi kufikiri kufika hapa katika maisha yangu, bila ushirikiano wa wachezaji wenzangu na kocha wangu hakika nisingeweza kufika hapa. Shukrani zangu kwa familia na ndugu zangu kwa ushirikiano walionipa katika safari yangu ya soka,” alisema Nadine.

Bao bora la mwaka ‘Puskas Award’
Nyota wa Colombia, James Rodriguez, aliibuka kinara wa bao bora la mwaka akiwapita, Stephanie Roche na mshambuliaji wa Manchester United, Robin Van Persie.

Rodriguez alipata jumla ya asilimia 42 akifuatiwa na Roche aliyepata asilimia 33 na mshambuliaji wa Man United akiambulia nafasi ya tatu kwa kupata jumla ya asilimia 11 ya kura zote zilizopigwa.

Kocha bora wa wanaume
Kocha wa Ujerumani,Joachim Low (54) ametwaa tuzo ya kuwa kocha bora wa mwaka akiliongoza taifa la Ujerumani kutwaa taji la dunia lililofanyika nchini Brazil, kwa kuichapa Argentina bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.

“Ni heshima kubwa kwangu kwa mafanikio haya niliyoyafikia, nafahamu michuano ya Kombe la Dunia ndio iliyonifikisha hapa hivyo napenda kuchukua tuzo hii kwa niaba ya wote walioshiriki katika kuweka mafanikio ya timu yetu ya taifa ya Ujerumani. Ahsante kwa wachezaji na familia yangu kwa ushirikiano wao kwangu,” alisema Loew.

Kocha bora wa wanawake
Kocha wa klabu ya Wolfsburg Ralf Kellermann (46) amechaguliwa kuwa kocha bora kwa upande wa soka la wanawake akifanikiwa kuiongoza klabu hiyo kutetea taji lao la Ulaya.

“Tuzo hii imekuja wakati muhimu sana kwangu, napenda kutoa shukrani kwa wachezaji na mashabiki wa timu yangu ya Wolfsburg, ni tuzo yetu wote kwa kuwa wote tulikuwa sehemu ya mafanikio,” alisema Kellerman.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles