BAADA ya kukiongoza vema kikosi cha Real Madrid, nyota wa timu hiyo, James Rodriguez, jana alifunguka akidai anajifunza mengi kupitia kwa kocha wake, Zinedine Zidane.
Rodriguez aliweka bayana mafanikio yake hasa baada ya juzi kuisaidia timu yake katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Espanyol.
Nyota huyo ambaye akuwahi kucheza tangu msimu uanze, alisaidia timu yake kuweka rekodi ya kushinda michezo 16 dhidi ya wapinzani wao katika michezo ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.
Timu hiyo ilishinda mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Estadi Cornella-El Prat bila ya washambuliaji wake, nyota Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.
Mcolombia huyo anahaha kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo licha kubainisha kutokupangwa katika kikosi hicho, anajifunza vitu vingi kutoka kwa kocha wake.
“Zidane ni kocha ninayejifunza mambo mengi kutoka kwake kwani kucheza timu hii ni ndoto yangu na natumaini nitaendelea kufanya vizuri.
“Familia yangu kwa pamoja, tuna furaha kuwapo hapa Madrid na kucheza kwenye timu hii, nitapambana nibaki hapa,” alisema.
Nyota huyo alisema si kweli yupo katika wakati mgumu ndani ya timu hiyo ingawa mara kadhaa hushindwa kuzungumzia hali hiyo mara kwa mara pindi anapoulizwa.
“Sisi tumejumuika kama timu na kila mmoja wetu ana mchango katika timu hii tangu aliposajiliwa na klabu, hivyo tunahitaji kushinda zaidi ili tuweke rekodi nyingi.
“Ninaelewa kuhusu maamuzi ya kocha, Zidane anaelewa kila wakati nataka kuisaidia timu si tu kufunga na kusaidia bao lipatikane,” alisema Rodriguez.
Nyota huyo alionesha kiwango kizuri katika mchezo huo kipindi cha kwanza na kusaidia vema na Karim Benzam aliyefunga bao la pili.
“Tulikuwa katika kiwango bora kipindi cha kwanza na tulipambana kutafuta ushindi,” alisema.