Na PATRICIA KIMELEMETA – Dar es Salaam
BAADA ya kuwapo kwa mjadala wa muda mrefu wa Tanzania kuibiwa dhahabu kutokana na mchanga wake kusafirishwa nje ya nchi, leo ukweli unatarajiwa kujulikana wakati kamati iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli itakapokabidhi ripoti yake.
Machi 29, mwaka huu, Rais Magufuli aliunda kamati yenye watu wanane, ambayo ilipewa jukumu la kuchunguza na kubaini kiwango cha madini kilichomo katika makontena yenye mchanga wa madini yanayoshikiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ni Profesa Abdulkarim Mruma na wajumbe wake ni Profesa Justianian Ikingula, Profesa Joseph Bushweshaiga, Dk. Yusuf Ngenya, Dk. Joseph Philip, Dk. Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.
Kamati hiyo iliundwa ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Rais Magufuli kutangaza kuzuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kuanzia Machi 2, mwaka huu, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta makontena 20 ya mchanga huo yakitaka kusafirishwa nje ya nchi.
“Nataka niwaambie nchi yetu inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena kama yapo, na kweli nimeyaona, sasa utaratibu utakapokamilika nataka Watanzania na dunia nzima ione kilichomo humu ndani kama ni mchanga kweli ama dhahabu,” alisema Rais Magufuli.
Jana Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, alitoa taarifa kwa umma ikisema kamati iliyoundwa kuchunguza mchanga huo, itamkabidhi Rais Magufuli ripoti yake leo kuanzia saa 3:30 asubuhi.
“Kamati maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli kwa ajili ya kuchunguza makontena ya mchanga yaliyokamatwa bandarini, itawasilisha ripoti yake leo kwa Rais,” alisema Msigwa.
Awali mara baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku mchanga kusafirishwa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitembelea mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mjini Kahama, na kuchukua sampuli ya mchanga wa dhahabu kuupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili aupime na kuona kuna aina ngapi na kiasi gani cha madini kinachopatikana.
Pia Machi 28, Rais Magufuli alimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote inayosababisha nchi kukosa mapato makubwa, hususani katika misamaha ya kodi, mikataba na ulipaji wa kodi.
“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili Watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa?” alisema Rais Magufuli.
Itakumbukwa kuwa mara baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga huo nje ya nchi, baadhi ya watu walitoa mawazo kinzani juu ya hatua hiyo, huku wengine wakiunga mkono.
Mmoja wa watu waliotoa maoni ni Mbunge wa Igunga na Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Dk. Dalali Kafumu, ambaye alisema suala la kuhakikisha Tanzania inachenjua madini yote nchini ni sahihi kwani ni la kisera.
“Sera ya madini ya mwaka 2009 niliyosimamia utengenezaji wake, kifungu 5.11; policy statement no. 3 inasema hivi: (iii) The Government will collaborate with the private sector, regional and international organizations to strategically invest in smelting and refining.
“Kwahiyo mchakato wa kuchenjua mchanga hapa nchini ni matakwa ya kisera, lakini shida inakuja tu pale ambapo shughuli hii inaanzishwa kwa haraka na dharura kubwa. Hali hiyo inaweza kuleta uhusiano usio sawa na makampuni ya kimataifa na hata nchi makampuni yanakotoka,” alisema.