Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakati ikiwa siku ya pili, ya Jukwaa la Kimataifa la Msaada wa Kisaikolojia (PSS FORUM), Mkurugenzi Wa REPSSI Tanzania, Edwick Mapalala ametumia nafasi hiyo kumuelezea baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI) ni shirika lenye makao makuu nchini Afrika Kusini, likijihusisha kwenye masuala ya malezi, makuzi na saikolojia hasa ya watoto katika nchi zaidi ya 13, Tanzania ikiwemo.
Katika siku ya pili ya Jukwaa la Kimataifa la shirika hilo, Mapalala amesema Tanzania inakila sababu ya kujivunia uwepo wa amani iliyoasisiwa na baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
“Kuna nchi siku moja nilikuwa huko, ikatokea kuna binti amevamiwa na kibaka, tukaogopa kusaidia lakini kuna walinzi pembeni tuliwaomba wamsaidie, wakauliza kwani yule binti kabila gani?” amesema na kuongeza;
“Tanzania hatuulizani kuhusu ukabila, tuna amani, unajua thamani ya kitu ukiwa nacho huwezi kuiona. Utaiona pale ukipoteza kitu hicho,” amesema.
Jukwaa la Msaada wa Kisaikolojia linafanyika wakati dunia ikikubwa na changamoto ya UVIKO – 19 jambo lililosababisha liendeshwe kwa njia ya mtandao.
Wadau wa masuala ya watoto na msaada wa kisaikolojia wakiwemo maafisa ustawi wa jamii kutoka Tanzania, wanashiriki jukwaa hilo wakiwa katika Hoteli ya Ramada, jijini Dar es Salaam.