29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Rekodi ya Ndanda yaitesa Azam

STEWART HALLNA ABDUCADO EMMANUEL, MTWARA

LICHA ya kuwa na matokeo mazuri hadi sasa, Mabingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), Azam FC, wameingiwa hofu katika mchezo wao wa leo dhidi ya Ndanda FC utakaofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini hapa.

Kocha wa Azam, Stewart Hall, ameliambia gazeti hili kuwa Ndanda si timu ya kubeza hasa kutokana na rekodi yake msimu huu ya kutopoteza mchezo wowote katika uwanja wao wa nyumbani hivyo watakuwa wamepania kuendeleza rekodi hiyo mbele ya Azam.

Alisema mchezo utakuwa mgumu sana na anatarajia kupata upinzani wa hali ya juu kutoka kwa Ndanda ambao msimu uliopita walikuwa timu ya kwanza kutibua mipango ya Azam ya kutokufungwa katika mechi zake za Ligi Kuu walipokutana katika uwanja huo.

Azam wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kati ya michezo sita waliyocheza hadi sasa wakishinda mitano na kutoka sare mmoja dhidi ya Yanga na kujikusanyia jumla ya pointi 16.

“Ndanda ni timu nzuri, hatuwezi kuibeza hata kidogo kwani imecheza mechi zake na kupata matokeo mazuri katika uwanja wake, tutakuwa na tahadhari kubwa kuhakikisha tunacheza kwa nidhamu ili tupate ushindi ingawa najua wazi mchezo utakuwa mgumu,” alisema Hall.

Kocha huyo raia wa Uingereza, alisema katika mechi hiyo atawakosa nyota wake wanne wakiwemo kipa namba moja, Aishi Manula ambaye ni majeruhi na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Hall ambaye amekuwa na kawaida ya kuwalalamikia waamuzi, alisema anaamini watachezesha kwa umakini kwa kufuata sheria 17 za soka.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo ambazo zinatarajiwa kuchezwa leo, Mwadui inayonolewa na kocha mwenye maneno mengi, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, itakuwa na kibarua cha kutafuta pointi muhimu watakapowakaribisha Mgambo JKT, huku Mbeya City wakiwa wenyeji wa African Sports katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Mchezo kati ya Mwadui na Mgambo JKT unatarajiwa kuwa mkali kutokana na timu hizo kuwa na pointi 11 kila moja ambapo timu itakayoshinda itajiwekea mazingira ya kubaki nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

Kwa upande wa Mbeya City na African Sports kila timu itakuwa na kazi kubwa kutokana na kutopata matokeo mazuri katika michezo yao iliyopita.

Katika mechi saba walizocheza Mbeya City wameshinda mchezo mmoja, sare mmoja na kupoteza michezo mitano na kufikisha pointi nne huku African Sports wakishinda mchezo mmoja na kupoza mitano na kujikusanyia pointi tatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles