27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yaua, Simba yafa

1.*Stand United yazidi kupeta, Coastal Union yazinduka

NA WAANDISHI WETU

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, jana waliendeleza ubabe katika ligi hiyo baada ya kuifanyia mauaji Toto Africans kwa kuifunga mabao 4-1 huku mahasimu wao, Simba wakilala kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Ushindi wa jana kwa Yanga ambao wamecheza mara moja ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na kushinda mabao 2-0 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, ni wa sita kwa vinara hao katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kuendelea kutesa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 19 huku ikiwaacha kwa mbali watani wao wa jadi Simba ambao wameshuka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 15.

Stand United wamefanikiwa kufikisha pointi 15 sawa na Simba na kuishusha hadi nafasi ya nne baada ya jana kuifunga Majimaji ya Songea mabao 3-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga lakini wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Elius Maguli, aliendeleza kasi yake ya kupachika mabao baada ya kuifungia timu yake mabao mawili dakika za 48 na 60 huku Pastory Pato akihitimisha kwa kufunga bao la tatu dakika ya 68.

Simba wameshindwa kuishusha Yanga kileleni na kuwaacha katika upinzani mkali na Azam FC ambao wanatarajiwa kuvaana na Ndanda FC leo katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Yanga waliokuwa wenyeji wa Toto, walianza kwa kasi pambano hilo jana na kufanya shambulizi kali dakika ya kwanza kupitia kwa mshambualiaji wake, Amissi Tambwe, lakini shuti hafifu alilopiga akiunganisha pasi ya Juma Abdul liliokolewa kirahisi na kipa Musa Mohamed.

Dakika ya nane Abdul alifanikiwa kuandika bao la kuongoza kwa Yanga baada ya kupiga shuti kali lililotinga nyavuni akiunganisha vyema mpira wa kona iliyochongwa na kiungo mchezeshaji, Haruna Niyonzima.

Toto walijibu mapigo kwa kufanya shambulizi kali dakika ya tisa kupitia kwa Miraji Athumani aliyeachia shuti lililopitiliza moja kwa moja pembeni mwa lango la Yanga na kutoka nje.

Mshambuliaji kinda wa Yanga, Godfrey Mwashiuya, alifanya uzembe na kukosa bao la wazi dakika ya 30 baada ya kutengeneza nafasi nzuri ya kufunga lakini akatoa pasi kwa Donald Ngoma na mpira kutua mikononi kwa kipa.

Yanga walizidisha mashambulizi langoni kwa Toto na dakika ya 44 walipata penalti baada ya mchezaji, Karlos Protas wa Toto kushika mpira uliopigwa na Ngoma akiwa katika harakati za kuokoa.

Hata hivyo, kipa Mohamed wa Toto alidhihirisha ubora wake baada ya kuidaka penalti hiyo iliyopigwa na Ngoma na kuwawadhibiti vilivyo Yanga kipindi cha kwanza licha ya kukabiliwa na tatizo la umaliziaji.

Kiungo Simon Msuva aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Abdul, aliifungia Yanga bao la pili baada ya kuachia shuti la mbali akiwa nje ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Toto

Hata hivyo, dakika ya 55, Japhet Vedastus wa Toto  aliifungia timu yake bao kwa mpira wa kichwa baada ya kutokea piga nikupige langoni kwa Yanga na kuwachanganya mabeki.

Dakika ya 81, Tambwe aliongeza bao la tatu kwa Yanga baada ya kutumia makosa ya kizembe yaliyofanywa na mabeki wa Toto na kuachia shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari.

Msuva alihitimisha karamu ya mabao kwa Yanga kwa kuandika bao la nne dakika ya 89 baada ya kufanikiwa kuunganisha vyema pasi ya Andrey Coutinho aliyeonyesha kiwango cha uhakika katika mchezo huo.

Mwamuzi wa mchezo huo, Ahmada Simba wa Kagera, alimuonya kwa kadi ya pili ya njano na kumtoa nje Hassan Khatib wa Toto aliyemfanyia madhambi Haji Mwinyi wa Yanga.

Kwa upande wa Simba waliokaribishwa na maafande wa Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, walijikuta wakichezea kichapo cha bao 1-0 na kushindwa kufikia malengo yao ya kuondoka na pointi sita kwenye uwanja huo.

Bao lililofungwa na Mohamed Mkopi dakika ya 61, lilitosha kuizamisha Simba na kuinyima pointi muhimu baada ya Jumamosi iliyopita kufanikiwa kuichapa Mbeya City bao 1-0 kwenye Uwanja huo.

Coastal Union ambao wamemtimua rasmi kocha wao mkuu, Jackson Mayanja, ilizinduka katika ligi hiyo na kuichapa Kagera Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Bao la pekee na la ushindi kwa Coastal Union lilipachikwa wavuni na Ismail Mohamed dakika ya 13 akiunganisha krosi safi iliyochongwa na Ibrahim Twaha.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles