27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Rekodi ya 2010/11 huenda ikajirudia

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

LIGI Kuu ya Vodacom msimu huu imekuwa na utata mkubwa kutokana na ugumu uliogubika mbio za ubingwa.Mpaka sasa mzunguko wa pili wa ligi ukiwa unaendelea, bado ni vigumu kutabiri ni timu gani inaweza kutwaa ubingwa.Kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo kuna vita kali baina ya mabingwa watetezi Azam FC na Yanga, wote wakiwa na pointi 25 baada ya kushuka dimbani mara 13, lakini Azam FC wako juu kutokana na uwiano wake mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kagera Sugar inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 21, lakini iko mbele michezo miwili baada ya kucheza mechi 15, huku pia ikiizidi Simba yenye pointi 20 kwa mchezo mmoja. Mabingwa hao wa zamani wa ligi wapo katika nafasi ya nne.

Kama Azam FC na Yanga zitafanya vibaya kwenye mechi zao mbili wiki hii, basi zinaweza kutoa mwanya kwa timu za Kagera Sugar na Simba zinazoikaribia kuwafikia.

Azam itacheza na Ruvu Shooting kesho katika Uwanja wa Mabatini, uliopo mkoani Pwani, kabla ya kupambana na Tanzania Prisons Jumapili hii Uwanja wa Azam Complex, uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, huku Yanga ikichuana na Prisons kesho na kumalizia mechi inayotazamiwa kuwa ngumu dhidi ya Mbeya City Jumapili, ambapo mechi zote zitachezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Ili kudhihirisha ugumu wa ligi, Simba kabla ya kucheza mchezo wake uliopita dhidi ya Polisi Morogoro ilioshinda mabao 2-0, ilikuwa ikikamata nafasi ya tisa, lakini baada ya ushindi huo ilipanda kwa nafasi tano hadi nafasi ya nne.

Mvutano mwingine upo baina ya timu zinazoshika nafasi ya tano hadi ya tisa ambazo ni Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting, Coastal Union, JKT Ruvu na Polisi Morogoro, kutokana na timu hizo zote kuwa na pointi 19.

Kama Simba na Kagera Sugar zitashindwa kuchanga vema karata zao katika mechi zijazo, basi zinaweza kujikuta zikiteremka hadi nafasi ya tisa na 10, hii itatokana na matokeo mazuri watakayopata timu hizo nne zilizo chini yake.

Timu ya Tanzania Prisons inayoburuta mkia kwa pointi 11, inazidiwa pointi 14 tu na vinara Azam FC, Prisons imeshinda mechi moja tu, kutoka sare nane na kufungwa mechi nne.

Msimu huu zitashuka daraja timu mbili tu ambapo kwenye vita hiyo zipo Prisons, Mgambo JKT (zote zenye pointi 14), Stand United (pointi 15), Ndanda (pointi 16) na Mbeya City (pointi 17), ambazo nazo zimepishana pointi chache sana.

Inakumbushia yaliyojiri 2010/11 Katika misimu ya hivi karibuni, msimu wa 2010/11 bingwa aliamuliwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwenye mechi za mwisho za ligi.

Kama zilivyo Azam FC na Yanga zinazokabana koo kileleni msimu huu, Simba na Yanga kwenye msimu huo zilikuwa zikilingana kwa pointi hadi mechi za mwisho.

Yanga ndio walikuwa mabingwa msimu huo baada ya mechi ya mwisho kuichapa Toto Africans mabao 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku Simba ikiichapa mabao 4-1 Majimaji, mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru na wote kufikisha jumla ya pointi 49.

Wanajangwani hao walikuwa mabingwa kufuatia kuwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (goal difference) ya 22, wakati Simba ikiwa na 21, cha kukumbukwa zaidi ni Emmanuel Okwi kukosa penalti kwenye mchezo huo dhidi ya Majimaji.

Hivyo kutokana na hali hiyo iliyopo msimu huu, huenda bingwa wa ligi akaamuliwa kwenye mchezo wa mwisho kwa staili kama ya msimu wa 2010/11.

Vita ya ufungaji bora

Mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu, raia wa Burundi, anaongoza kwenye chati ya ufungaji bora akiwa na mabao tisa katika mechi 13 alizocheza msimu huu.

Mchezaji bora wa ligi msimu uliopita, Kipre Tchetche (Azam FC), anakabana koo na Ame Ally (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar) na Samuel Kamuntu (JKT Ruvu), wote wakiwa wamefunga mabao sita.

Vita hiyo ni kubwa, ili Kavumbagu aweze kujihakikishia kukitwaa kiatu hicho lazima ahakikishe anaendelea na kasi yake ya ufungaji, kwani mpaka hivi sasa zimebakia takribani mechi 12 ligi kumalizika.

TPLB yafurahishwa

MTANZANIA lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Hamad Yahya, kuzungumzia ushindani huo ambapo alisema msimu huu umekuwa wa kihistoria ikilinganishwa na misimu mingine.

“Zamani timu za mikoani zilizoeleka kuchagua idadi ya mabao ya kufungwa wanapokuja Dar es Salaam, lakini hivi sasa hali imekuwa tofauti, baada ya ligi kuwa na ushindani mkubwa,”

“Huu umekuwa msimu wa kihistoria sana tofauti na misimu iliyopita na ushindani huu umechangiwa na fedha nyingi inazopata timu kutoka kwa wadhamini wa ligi,” alisema.

Alisema kutokana na wingi wa fedha Ligi Kuu Bara, hakuna timu inayotaka kushuka daraja kirahisi, hali inayopelekea kuonyesha ushindani uwanjani ili kupata matokeo mazuri.

Kila timu imekuwa ikivuna takribani Sh milioni 170 kwa msimu kutoka kwa mdhamini mkuu wa ligi (Kampuni ya Vodacom) na mdhamini wa matangazo ya televisheni (Azam TV).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles