27.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

Sitta, Bodi wasigana kuhusu mkurugenzi mpya ATCL

Pg 3Na Michael Sarungi, Dar es Salaam
WAZIRI wa Uchukuzi, Samweli Sitta na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wametofautiana kauli kuhusu atakayebeba mikoba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Kapteni Lazaro Militon ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria, Februari mosi mwaka huu.
Tofauti hizo zilibainika jana baada ya Waziri Sitta kuliambia MTANZANIA kuwa hana taarifa za uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi mpya wa ATCL, Jonson Mfinanga, huku Bodi ya shirika hilo ikitoa taarifa kwenye vyombo vya habari kuhusu uteuzi huo.
“Taarifa nilizonazo mpaka sasa ni kwamba tayari Bodi imeandaa utaratibu wa kumuombea kwa mamlaka husika ili Kapteni Lazaro aongezewe muda.
“Kwa hiyo itategemeana na uamuzi wa mamlaka husika kama wataona anafaa basi watachukua uamuzi unaofaa,” alisema Sitta.
Alisema kwa kawaida Bodi ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha anapatikana mkurugenzi baada ya aliyekuwapo kumaliza muda wake kwa mujibu wa sheria au kwa sababu nyingine.
Sitta alisema mkurugenzi aliyemaliza muda wake amestaafu kwa mujibu wa taratibu za sheria na wala hapakuwapo masuala mengine zaidi ya hilo.
MTANZANIA lilipowasiliana na Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Salim Msoma kupata ufafanuzi wa suala hilo, kauli yake ilipingana na ya Waziri Sitta.
Msoma alisema Bodi yake ilikwishakaa wiki moja iliyopita na kumpata mrithi wa Lazaro.
“Ni kweli mkurugenzi wa zamani amestaafu kwa mujibu wa sheria na tayari utaratibu wa kumpata mkurugenzi mpya ulikwisha kufanyika na kumpata.
“Tuna uongozi mpya na kama unataka uthibitisho nenda kwenye ofisi yetu utamkuta akiendelea na kazi ya kuhakikisha shirika linarudi katika hali yake ya kawaida,” alisema Msoma.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya kumaliza kazi hiyo bodi kwa kushirikiana na wadau wengine itahakikisha inapambana na changamoto zote zinazolikabili shirika kwa lengo la kulirudisha katika hali yake ya kawaida.
Aliwataka wafanyakazi wa shirika hilo kumpa ushirikiano wa kutosha kaimu mkurugenzi mpya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles