26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

RC, wizara watofautina juu ya kipindupindu

said meck sadikNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick ametofautiana na watendaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto juu ya taarifa ya kuwapo ugonjwa wa kipindupindu mkoani humo.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Sadick alisema watendaji hao wametoa taarifa ambazo si sahihi kwa viongozi wa wizara hiyo, kuwa ugonjwa huo umerejea tena.

“Watendaji wametoa taarifa ya uongo… hakuna ugonjwa wa kipindupindu Dar es Salaam, unajua mtu akianza kutapika ovyo tunachukua tahadhari ya kumuweka kwenye kambi kwa ajili ya vipimo, sasa wao hawasubiri vipimo wanapeleka taarifa kuwa kuna wagonjwa.

“Na kama ulifuatilia vizuri taarifa ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, alisema watu waliokuwa wamelazwa katika kambi maalumu ya wagonjwa wa kipindupindu waliwabaini kuwa hawaugui ugonjwa wa kipindupindu.

“Na hii si mara ya kwanza, kuna siku pia wafanyabiashara wawili walitoka Mwanza waliposhuka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) walianza kutapika, walipopelekwa kambini walisema ni wagonjwa wa kipindupindu, baadae ilibainika hawakuwa na ugonjwa huo,” alisema.

Sadick aliwataka watendaji wanaopita kukusanya taarifa juu ya ugonjwa huo kuwa makini, na kwamba ni vema wakasubiri uthibitisho wa vipimo kabla ya kupeleka taarifa,” alisema.

Hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema ugonjwa huo unapaswa kudhibitiwa na kwamba watendaji wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya ambao ugonjwa huo utaendelea kuripotiwa katika maeneo yao watawajibishwa.

“Watendaji ambao ugonjwa wa kipindupindu utaendelea kuwapo kwenye maeneo yao watawajibika, tunataka taarifa hizi tuzitoe kila wiki kwa wananchi na wadau ili tujue hali halisi,” alisema.

Aliwataka kusimamia sheria na kanuni za usafi, ikiwamo kudhibiti uuzwaji wa matunda yaliyokatwa pamoja na vyakula kwenye maeneo ya wazi.

Katika hatua nyingine, kuhusu kufuta safari za madiwani wa manispaa za jiji hilo, Sadick alisema hatua hiyo imefikiwa ili kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika na kuzipeleka kwenye sekta ya elimu.

“Nimefuta safari za ndani na nje za madiwani na watendaji pamoja na mikutano ambayo haina  ulazima pamoja na kuondoa viburudisho, hatua hiyo imesaidia kuokoa Sh bilioni 4.6 ambazo nimezielekeza kwenye sekta ya elimu.

“Kuna matatizo makubwa ya ukosefu wa madawati, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, kwahiyo tutatumia fedha hizi kuzitatua,” alisema.

Kuhusu kuongezeka idadi ya manispaa za jiji hilo kutoka tatu hadi tano, alisema hatua hiyo imelenga kusogeza huduma kwa wananchi.

“Manispaa ya Temeke imegawanywa na kutoka nyingine ya Kigamboni, pia Kinondoni imegawanywa na kuanzisha nyingine ya Ubungo. Ile ya Ilala inabaki vilevile, tumelenga kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles