Na Clara Matimo, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amepiga marufukj matukio yote yasiyo ya lazima yanayosababisha mikusanyiko lengo likiwa ni kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa corona.
Pia amewasisitiza wakazi wa mkoa huo kufuatilia kwa makini elimu inayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa corona.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Julai 20, 2021, Mhandisi Gabriel amezitaka Mamlaka zinazohusika kutoa vibali vya mikusanyiko kusitisha katika kipindi hiki ambacho mkoa unaendelea kupambana ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona.
“Mikusanyiko isiyokuwa na sababu yoyote hakuna sababu ya kutoa vibali kipindi hiki tuko kwenye kampeni ya kumlinda mwana Mwanza, usalama wa maisha kwanza, mengine yanakuja baadaye.
“Vikao vinakuja baadaye, mikutano inakuja baadaye, siasa zinakuja baadaye na matamasha yanakuja baadaye lakini kwanza ni usalama wa maisha yetu,”alisisitiza.
Amesema matukio ambayo siyo ya lazima yanayosababisha mikusanyiko hayataruhusiwa kabisa ila ibada ma misiba iendelee lakini kwa uangalizi wa hali ya juu.
“Nasisitiza wananchi kuvaa barakoa wanapokuwa kwenye mikusanyiko ya lazima kama nyumba za ibada na kwenye msiba pia kila mtu ahakikishe ananawa mikono ama atumie vitakasa mikono pamoja na kuhakikisha anakaa mbali na mtu mwingine tukitimiza hayo tutakuwa tunaendelea kujilinda,” alisema na kuongeza;
“Katika mkoa etu tumetenga wiki moja kwa ajili ya kuuombea mkoa wetu Mwenyezi Mungu atuepushe na ugonjwa huo, kila mmoja kwa dini yake na kwa muda wake aombe kwelikweli maana Mungu ndiye tegemeo letu,” amesema.