Florence Sanawa – Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, amewahimiza wakazi wa mkoa huo kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara baada vijana 12 kati ya 325 kukutwa na maambukizi ya magonjwa ya ini walipofanyiwa vipimo katika usaili wa kujiunga na jeshi la kujenga Taifa (JKT), mkoani humo.
Akizungumza katika kikao cha ushauri cha mkoa (RCC), amesema endapo wananchi watakuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara na kuanza kukabiliana na magonjwa hayo hayataweza kutuathiri kwa kiasi kikubwa kwakua watapata tiba mapema.
Akizitaja wilaya zilizo bainika kuwepo wa vijana wenye maambukizi ya ugonjwa wa ini Bykanwa amesema ni Wilaya ya Nanyumbu ambapo vijana 10 wamebainika kuwa ugonjwa huo na Wilaya ya Newala ambapo vijana wawili wamekutwa na ugonjwa huo.
“Ugonjwa wa ini ni miongoni mwa magonjwa yanayoathiri jamii nyingi za kitanzania ambapo serikali imekuwa ikipigia kelele kwa taasisi mbalimbali zinazo jihusisha na afya kujikita katika kutoa elimu kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao na kuweza kuzikabili hasa kwa wale walio bainika,” amesema.