SERIKALI mkoani Kilimanjaro imezijia juu halmashauri mbili za wilaya za Siha na Moshi, baada ya kushindwa kutumia fedha za miradi ya barabara katika kipindi cha mwaka wa fedha uliomalizika wa 2015/ 2016.
Akizungumza katika kikao cha kwanza katika mwaka mpya wa fedha wa 2016/2017 cha bodi ya barabara mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, alisema halmashauri hizo zimefanya uzembe wa kutozitumia fedha za utekelezaji wa miradi ya barabara ambazo ni zaidi ya Sh milioni 100.
Alisema kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Siha ilibakisha Sh milioni 58 huku Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ikibakisha Sh milioni 52.
“Kitendo hicho kilichofanywa na wakurugenzi wa halmashauri hizo kimesababisha kutokamilika kwa miundombinu ya barabara na kusababisha wananchi kupata kero ya barabara ikiwamo wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao na kuendelea kudidimiza uchumi.
“Wakati wananchi wanateseka kwa kukosa miundombinu bora ya barabara, halmashauri hizo zimebakisha fedha za ujenzi wa barabara na jambo hili ni la aibu.
“Kutokana na hali hiyo, wakurugenzi na wahandisi wote wa wilaya lazima mhakikishe mnakamilisha taratibu za manunuzi mapema kabla mwaka wa fedha haujamalizika.
“Nayasema haya kwa sababu baadhi ya wakurugenzi na wahandisi wa wilaya mmekuwa wazembe katika kukamilisha taratibu za manunuzi, jambo ambalo limekuwa likisababisha fedha nyingi za miradi ya maendeleo kutotumika kama ilivyokusudiwa.
“Sasa nawaambia wazi, kuwa mimi sitaivumilia halmashauri itakayofanya hivyo wakati wananchi wanateseka kwa kukosa maendeleo,” alisema
Sadiki.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya barabara mkoani hapa, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Kilimanjaro, Ntije Nkolante, alisema hadi sasa zaidi ya Sh bilioni 8.7 zimeidhinishwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara.