UPENDO MOSHA-MOSHI
SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro, kuweka mfumo mzuri wa udhibiti wa ukwepaji kodi na biashara za magendo katika maeneo ya mipaka ya Holili na Tarakea.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Kilimanjaro, Anna Mgwhira, wakati akizungumza na baaadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo katika uzinduzi wa Wiki ya Mlipakodi iliyofanyika mjini Moshi mkoani hapa.
Alisema kwamba, baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia njia za panya kupitisha biadhaa za magendo katika Mipaka ya Holili na Tarakea, jambo ambalo limekuwa likiisababishia Serikali hasara kwa kupoteza mapato yake.
“TRA mkoani kwetu hapa bado mna wajibu wa kubuni mbinu na njia mbalimbali za kukabiliana na tatizo la biashara za magendo mipakani pamoja na ukwepaji wa kodi.
“Lazima mhakikishe mnawachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara watakaobainika kufanya matendo haya maovu.
“Sambamba na hilo, TRA mzingatie kuongeza ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali na vyombo vingine katika kupiga vita ukwepaji wa kodi na magendo,” alisema Mghwira.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, vitendo vya ukwepaji kodi vinachangia kukwamisha malengo na mipango ya maendeleo ya Serikali, hivyo vinapaswa kudhibitiwa.
“Imarisheni ukaguzi wa kumbukumbu za walipa kodi ili kutambua kodi iliyokwepwa na hakikisheni pia kila mwananchi anatambua umuhimu wa kulipa kodi na mifumo hiyo iwe wazi,” alisema.
Naye Kaimu Meneja wa TRA, Mkoa wa Kilimanjaro, Rashid Herith, alisema makusanyo ya kodi yameongezeka kwa mwaka 2017/18 ambapo walifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 1.7 ikilinganishwa na mwaka 2016/17 ambapo walikusanya zaidi ya Sh bilioni 1.5.