Na Waandishi Wetu-ARUSHA
JESHI la Polisi mkoani Arusha limewakamata viongozi wa Shirikisho la Wenye Shule na Vyuo Binafsi nchini waliokuwa wamekwenda kutoa rambirambi kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent waliofariki dunia kwa ajali ya basi hivi karibuni.
Wengine waliokamatwa ni Meya wa Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro ,waandishi wa habari 10 kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliokuwa wakifuatilia tukio hilo,viongozi wa dini wanne, Mkuu wa Shule na Diwani wa Kata ya Olasiti.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Yusufu Ilembo, alithibitisha kuwa amri ya kuwakamata viongozi na waandishi wa habari wakati wakitekeleza majukumu yao, ni agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Tukio hilo lilitokea jana saa 11:49 katika shule hiyo wakati Mchungaji Joannes Mujungu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Olasiti, alipokuwa akisali kabla ya viongozi kuanza kuwasilisha michango yao kwa wazazi.
Waandishi waliokamatwa na vyombo wanavyotoka kwenye mabano ni Janeth Mushi (MTANZANI), Iddy Uwesu (Azam TV),Godfray Thomas (AYO TV), Filberth Rweyemamu (Mwananchi), Zephania Ubwani (Citizen), Husein Tuta (ITV), Josefu Ngilisho (Sunrise Redio), Elihuruma Yohana (Tanzania Daima ) na Alphonce Kusaga (Redio Triple A) .
KABLA YA KUKAMATWA
Awali, kabla ya kukamatwa viongozi hao, Meya Lazaro, alisema shirikisho hilo lilikuwa limetuma wawakilishi kwa ajili ya kuwasilisha rambirambi zao kwa wazazi na watoto waliofariki dunia hivyo aliomba wazazi hao wakabidhiwe.
Aliwaomba wazazi na walezi hao kushiriki katika ibada maalumu inayotarajiwa kuongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Jimbo la Kaskazini Kati, Dk. Solomon Masangwa, kuwaombea waliofariki dunia na majeruhi wanaopatiwa matibabu Marekani.
Alisema Ijumaa wiki hii (leo), au wiki ijayo, itafanyika sala maalumu kuwaombea wanafunzi 32 waliofariki dunia,walimu wawili, dereva mmoja na majeruhi watatu.
“Nimeona nizikusanye na kutafutana ili kuzikabidhi, niliomba waitwe wazazi wenyewe ilete heshima zaidi,”alisema.
Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao, akiwasilisha taarifa, alisema walikubalina kuchanga Sh milioni 10 kwa ajili ya kutoa pole kwa wafiwa na familia za majeruhi wanaopatiwa matibabu Marekani.
“Hakuna senti ya mtu itaenda pembeni, hatumpi mtu kama siyo mzazi, wala shule, tuliona majeneza 35 na majeruhi watatu… kiasi hiki kitagawiwa kwa familia 38, watakaokuwapo hapa na wale ambao hawapo, shule itatupa utaratibu wa kuwafikia, kila mtu atapewa fedha mkononi,”alisema.
Alisema michango hiyo imetolewa na watu 139 na itawekwa wazi katika mitandao ya jamii baaada ya kukabidhi rambirambi hizo waliotoa fedha hizo wasione fedha zao zimeliwa na akawataka wazazi kuendelea kujipa moyo.
OC CID AVUNJA SALA
Wakati mchungaji huyo anamalizia kusali, polisi wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OC-CID), Damas Masawe, walifika shuleni hapo na kudai mkusanyiko huo haukuwa halali.
Makabidhiano hayo yalikuwa yakifanyika katika chumba cha darasa ambako ndiko walikuwa wamekusanyika watu hao.
Kutokana na Massawe kuingia katikati ya maombi hayo, kiongozi huyo wa dini alilazimika kukatisha sala.
Baada ya hapo, Massawe aliamuru askari waliokuwa wamevalia kiraia na wenye sare wakiwa na silaha, kuwaweka chini ya ulinzi watu waliokuwa ndani ya chumba hicho.
Alidai mkutano huo haukuwa na kibali na ni kinyume cha sheria, hivyo alikuwa anauvunja.
Alisema hata kama kuna mkutano wa taasisi za dini ni lazima kibali kiombwe kuonyesha lengo la mkusanyiko huo na mahali unapofanyika saa 48 kabla ya mkutano husika.
Massawe aliwataka polisi kuwatoa nje ya chumba hicho viongozi waliokuwa wamekaa meza kuu isipokuwa wazazi ambao waliokuwa zaidi ya 20, wakisubiri kupewa rambirambi hizo.
Baada ya kuwatoa nje viongozi hao, Damas aliwataka waandishi wa habari kutoka nje na kuamuru wote kila mmoja aandike jina lake mbele ya askari kanzu aliyekuwa nje ya darasa.
Baada ya kumaliza kuandika majina waandishi walipandishwa ndani ya magari mawili ya polisi ya Toyota Land Cruiser pamoja na viongozi hao.
Katika tukio hilo, polisi walikuwa na magari matatu ambayo yalikuwa yakiongozwa na pikipiki mbili, huku yakipiga honi yakiamuru magari mengine yageshwe pembeni kupisha ‘msafara’ huo.
Walipofikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, wote waliwekwa katika chumba cha mgahawa walikosubiri kwa zaidi ya saa moja na nusu ili kuhojiwa.
OC- CID waandishi waitwe ofisini kwake na walipofika, huku akiwa na askari kanzu zaidi ya 10, aliwaeleza kuwa waliamua kuwapa lifti hivyo wanaweza kuondoka kituoni hapo.
“Tuliwapa lifti tu maana tunajua hamna magari ili msije kutuomba lifti, ila kuna kitu tunataka kufuatilia, tunataka kujua ni mwandishi gani aliyewaalika katika tukio hilo maana tunajua huwa kuna anayewaalika katika shughuli hii,”alisema.
Baada ya maelezo hayo waandishi hao waliachiwa saa 7: 28 mchana bila masharti yoyote, huku meya na wenzake 12 akiwamo Katibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Innocent Kisanyaga, wakiendelea kushikiliwa mahabusu.
OC -CID
Awali, Massawe alipokuwa akiingia ofisini kwa Kaimu RPC, aliwaambia waandishi waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi hiyo wakisubiri kuingia ndani kuwa atawafuata katika nyumba zao mmoja moja iwapo wataandika habari ya tukio hilo.
“Atakayeandika kuhusu haya nitamfuata nyumbani kwake mmoja baada ya mwingine, “ alisikika akisema bila kufafanua, na kuwaacha waandishi wakiwa wamepigwa butwaa.
KAIMU RPC
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi, Yusufu Ilembo, alisema jeshi hilo lilipokea taarifa za kuwapo mkusanyiko usio halali katika eneo la Shule ya Lucky Vincent, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, jambo ambalo alidai lingeweza kuhatarisha amani.
“Kama mnavyofahamu suala hili bado lina shinikizo kubwa kutoka kila upande, lazima tuchukue tahadhari. Tulipokea maagizo kutoka kwa mkuu wa mkoa ambaye naye alisema alipigiwa simu na raia mwema kuwa ulikuwapo mkusanyiko usio halali.
“Kumbe Shirikisho la Shule na Vyuo binafsi walikuwa wamepanga kuwasilisha rambirambi zao kwa wafiwa na waathirika wa tukio la ajali iliyotokea. Katika msafara wao walifuatana na Meya wa Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro, viongozi wa dini na waandishi wa habari,” alisema Ilembo.
Kwa mujibu wa Ilembo, polisi wanachunguza tukio hilo kwa kuwahoji wote waliokutwa katika eneo la shule bila kuwa na kibali, huku wakiwa na kiasi kikubwa cha fedha kinyume cha utaratibu.
“Walikuwa na kiasi kikubwa cha fedha, Sh milioni 18, walikuwa waziwasilishe kama rambirambi zao lakini hawajampa taarifa mtu yeyote. Polisi hatukuwa na taarifa… fedha hizo zingeingia kwenye mikono ya watu wabaya.
“Vilevile wanafunzi walikuwa darasani kwa hiyo ilikuwa kama kusumbua na kuwakumbusha majonzi yaliyotokana na tukio la wenzao waliopata ajali na kufariki dunia,” alisema Kaimu Kamanda huyo.
APC
Akizungumza nje ya Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu alisema klabu hiyo italiandikia barua rasmi jeshi la polisi kujua sababu hasa za jeshi kuendelea kuwabughudhi waandishi wakitekeleza majukumu yao.
“Tunalaani kwa nguvu zote kitendo kilichofanywa na polisi cha kuwakamata wenzetu waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.
“Uongozi wa APC utaandika barua rasmi kuomba ufafanuzi wa tukio hili lisilokubalika kwa sababu uandishi ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine.
“Jambo lolote linalohusu taaluma hii linapaswa kushughulikiwa kwa utaratibu unaokubalika,” alisema Gwandu.
GAMBO
RC Gambo alipotafutwa kuzungumzia kama kweli alitoa amri ya kukamatwa viongozi hao, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.