25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 17, 2022

WABUNGE WAPINGA KITANZI CHA KODI KWA WAWEKEZAJI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


BAADHI ya wabunge, wamesema mazingira ya uwekezaji nchini, siyo mazuri kwa wawekezaji kutokana na kodi wanazotozwa.

Kutokana na hali hyo, wamesema Serikali inatakiwa kuangalia upya mazingira hayo ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.

Malalamiko hayo yalitolewa na wabunge hao jana walipokuwa wakijadili Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha  2017/18 iliyowasilishwa juzi na Waziri, Charles Mwijage.

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema kama hakutakuwa na  mabadikiko katika eneo hilo, uwezekano wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda ni mdogo.

“Kwanza kabisa nampongeza Rais Magufuli kwa kuwa na dhana ya Serikali ya viwanda kwa sababu hata mwaka 1967, Hayati Mwalimu Nyerere aliasisi dhana hiyo ingawa baadaye viwanda vilikufa.

“Mwaka jana nilionesha shaka yangu juu ya utekelezaji wa dhamira ya yeye kufikia yale ambayo alikuwa ametarajia na leo tunayaona.

“Vision (mtazamo) ya Rais ni kujenga uchumi wa viwanda utakaolijenga Taifa ili lijitegemee, lakini tuna tatizo kubwa la ku-link vision ya Rais na mikakati yetu ya kuweza kufikia malengo aliyonayo Rais.

“Katika hili, nataka nitoe mifano michache kwani hata taarifa ya BoT ya Aprili mwaka huu, inaonyesha manufacturing industries imeshuka kutoka Dola za Marekani milioni 1.4 hadi Dola za Marekani 870,000.

“Uzalishaji wa samaki nao umeshuka kwa Dola za Marekani milioni 20 na mikopo katika sekta ya kilimo imeshashuka hadi kufikia negative 92, usafiri na mawasiliano umeshuka kwa negative 21.6, ujenzi umeshuka kwa three negative na hoteli pamoja na migahawa, imeshuka kwa asilimia saba.

“Katika usafirishaji wa mazao, bidhaa pekee iliyokua ni korosho kutokana na kuongezeka kwa bei, lakini tumbaku imeshuka kutoka Dola za Marekani 343 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 281 mwaka huu.

“Pamba nayo imeshuka kwa Dola za Marekani milioni 10, kahawa imeshuka kwa Dola milioni tisa, karafuu kwa Dola milioni 13 na katani imekua kwa Dola za Marekani milioni moja.

“Capital goods nazo zimeshuka hadi negative 16.7, usafiri umeshuka kwa 23.9, ujenzi imeshuka kwa 19.3 na machinery imeshuka kwa 11.3.

“Tatizo lililopo ni sera za kodi tulizonazo na mfano halisi ni sheria ya uwekezaji, kifungu namba 19 cha sheria hii ambayo tumeibadilisha mwaka 2009, 2010, 2012, 2014 na 2015,” alisema Bashe.

Pamoja na hayo, Bashe alilalamikia taratibu za uwekezaji nchini kwa kusema kuwa zina usumbufu usiotakiwa kwa kuwa mwekezaji anatakiwa kwenda katika ofisi nyingi kupata vibali.

“Ili uwekeze kiwanda kidogo cha maziwa, unahitaji leseni kutoka Brela, unahitaji premise registration, equipment registration, product and testing  registration certificate, staff health certification,  ongoing inspection, import and export permit na ili uzipate hizi, zinatakiwa zipite Brela, TFDA, TBS, OSHA, Wizara ya Kazi na NEMC.

“Yaani hata kuzalisha square feet ya ngozi Tanzania ni Dola senti 14, Ethiopia ni senti nane, India ni senti saba na Pakistani ni senti nane.

“Kwa mazingira haya, nani atakuja kuwekeza hapa, je tutawezaje kushindana wakati sisi tumeweka export duty, how can we grow?,” alisema Bashe.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali iboreshe mifumo yake ya kodi ili kuwashawishi wawekezaji kwa kuwa wengi wao wanaiona Tanzania kama eneo lisilokuwa rafiki katika uwekezaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Maria Kangoye (CCM), alieleza jinsi Kampuni ya Own Care ilivyohamishia uwekezaji wake nchini Mauritius baada ya kutoridhishwa na masharti ya uwekezaji Tanzania.

Naye Mbunge wa Busega, Dk. Rafael Chegeni (CCM), alilalamikia wingi wa kodi na kusema katika sekta ya utalii, kuna kodi zaidi ya 36 wanazotakiwa kulipa wawekezaji.

Wakati huo huo, Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali (CCM), alilalamikia kodi kubwa inayotozwa katika ngozi kwa wawekezaji wa nje na kutaka ziondolewe ili wawekazaji hao waweze kuzinunua kwa urahisi.

Pamoja na hayo, wabunge hao waliitaka Serikali iondoe kodi hizo kwa sababu zinakwamisha wawekezaji. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,727FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles