UKIFIKA mkoani Dodoma hasa katika eneo la Nyerere Square, utakutana na kundi kubwa la ombaomba ambalo wana vichupa vidogo ambavyo ndani yake vimewekwa gundi kwa ajili ya kuvuta.
Sababu kubwa ya watoto hao kuwepo katika eneo hilo ni kutokana na kuwa na migahawa kwa ajili ya chakula.
Kundi hilo la ombaomba ambalo wengi ni watoto, mara baada ya kuvuta hupata usingizi na kulala moja kwa moja pembezoni mwa benki moja iliyo karibu na migahawa hiyo, sababu ikiwa ni gundi iliyowekwa katika vichupa hivyo.
Nimeshuhudia mara nyingi kundi hilo la ombaomba likiwa limekaa huku wakivuta gundi hiyo bila ya wasiwasi wowote.
Nani asiyejua kuwa gundi ikivutwa huwa ina madhara makubwa katika mwili wa mwanadamu?
Tunajua kuwa sifa kubwa ya Mkoa wa Dodoma ni kuomba, lakini hili la hawa watoto kuomba huku wakiwa wanavuta gundi halikubaliki.
Kwangu naliona ni jambo geni ambalo wahusika wanatakiwa waliangalie kwani tusipokuwa makini tutatengeneza kizazi kibaya hapo baadaye.
Lakini kuna hili pia la wazazi na walezi kuwatuma watoto wakaombe nalo silikubali.
Nirudi kwenye jambo langu la leo, hivi hawa vijana wanaovuta gundi katika eneo la Nyerere Square wahusika hamuwaoni.
Lakini kumekuwa na tuhuma kuwa mara baada ya kuvuta gundi hizo, vijana hao hulawitiana wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo ni baya na linasikitisha kwani wengi ni wanaume.
Naliweka hili mezani hivi mnaohusika jambo hili la ombaomba kutumia gundi pamoja na kulawitiana wenyewe kwa wenyewe hamlioni au kwa sababu hawana uwezo ndio mana mnaamua kuwaacha ili waangamie.
Nadhani umefika wakati wa kuchukua hatua kwa kuwakamata watoto wote wanaovuta gundi ili kukikomboa kizazi hicho.
Nasema ni watoto kulingana na umri wao kwani wengi wanaokaa katika eneo hilo ni watoto wanaotakiwa kwenda shule.
Matumizi ya gundi ni sawa na dawa za kulevya, kwani tumewashuhudia wale watoto baada ya kuvuta gundi huwa wanalala.
Kuna kijana mmoja aliniuma sikio katika kundi hilo hilo la ombaomba, kuwa hawataki kurudi makwao kutokana na kutokuwepo kwa gundi.
Aliniambia kuwa katika vichupa hivyo hujazwa mafuta ya petroli kidogo na gundi ya viatu ili waweze kupata stimu ya maisha.
Ananiambia hawezi kuacha na katika maisha yake hata akiwa na maisha ya aina gani, hajaona starehe zaidi ya kuvuta gundi.
Hapa ndipo nami ninapoanza kuhoji hawa wanaohusika hawawaoni hawa watoto jinsi wanavyovuta gundi tena mbele ya hadhara.
Nasema hili kutokana na kwanza, Mkoa wa Dodoma una tatizo la ombaomba halafu hao hao ombaomba tena wanavuta gundi, hebu nambie tunatengeneza taifa la aina gani?
Naumia kizazi kijacho kuwa cha ajabu zaidi ya hichi kutokana na wale wenye mamlaka kupuuzia mamlaka waliyopewa katika jamii.
Tunaona jinsi hawa watoto wakiwa wanazalishwa katika umri mdogo, huku wakiwatumia chambo watoto wao kuomba ili kuweza kujipatia kipato.
Tunajua kuwa eneo la Nyerere Square ni maalumu kwa ajili ya kupumzikia pamoja na kupata kumbukumbu ya Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Nyerere.
Lakini hili la hao watoto kufanya matukio hayo, sikubaliani kabisa kwa sababu eneo hilo ni kioo cha Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya nchi.
Pia watoto hao wamekuwa kero kwa wateja ambao wamekuwa wakila katika maeneo hayo kutokana na kuomba, lakini pia hata wakipewa hurudi kwa mara nyingine.
Serikali ya Mkoa wa Dodoma chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, hebu komesha tabia hii ya ombaomba.
Watoto ambao wengi tunasema ni taifa la kesho, sasa swali la kujiuliza tutatengeneza taifa la kesho kwa ombaomba au kwa kula gundi?