32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mliopewa dhamana mnamwangusha Rais Magufuli

magufuliNa DEOGRATIAS KISHOMBO

RAIS John` Magufuli amejitoa mhanga kuwaamini vijana katika kushika nyadhifa mbalimbali serikalini. Pengine ni Rais wa mfano, lakini cha kushangaza baadhi ya vijana hao wameanza kutia aibu.

Ni wazi kwamba wasaidizi wote waliopata dhamana ya kumsaidia Rais ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo wana wajibu wa kuisaidia Serikali iliyoko madarakani.

Kutokana na hilo, yule anayejaribu kukwamisha shughuli za kiserikali anatia doa chama kilichopewa dhamana na Watanzania.

Kilichotokea Kagera kwa Katibu Tawala wa Mkoa, Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda pamoja na Mhasibu Mkuu wa Mkoa, Simbaufoo Swai, kufungua akaunti kwa ajili ya kujipatia fedha za maafa kinyume na utaratibu ni kitendo cha kulaaniwa.

Wakati haya yakitokea, Serikali iko katika kupokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya wahanga wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Ni aibu kwa wasomi na vijana mliopewa dhamana na kuanza kutapeli watu ambao wako kwenye misiba ya kuomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao waliofariki katika tetemeko la ardhi lilitokea  Septemba 10, mwaka huu.

Kwa watu mliokula viapo vya uadilifu, mlioapa kuwajibika na kumwakilisha rais na kutimiza wajibu kwa mujibu wa maadili ya uongozi wa umma, mnaingia katika michezo ya kihuni na kitapeli inasikitisha.

Hiyo akaunti ya benki mliokuwa mmeifungua kutapeli michango kwa ajili ya wahanga wa tetemeko la ardhi, wananchi wa Kagera hasa kwa wale waliopoteza ndugu na jamaa ambao mpaka sasa hawajawapa msaada wowote watawalaani milele.

Hali ya wananchi Kagera ni tete. Bado waathirika wengi wanalia hawana msaada. Wananchi walio wengi maeneo ya mjini na vijijini wanalala nje. Hawana maturubai wala mahema.

Maeneo kama Maruku, Kiziba (Kanyigo), Minziro na sehemu za maeneo ya Manispaa ya Bukoba mjini wanalala nje, wana hofu na mvua ambazo zimeanza kunyesha.

Kwa mfano mratibu wa maafa wa Wilaya za Bukoba Mjini na Vijijini, Benetson Rwekamwa, anasema hali ni mbaya sana kwa watu hasa wanaoishi vijijini ambao hawana mahema wala maturubai

Vikongwe, walemavu na watoto wanahangaika. Watoto wanaleana baada ya kupoteza wazazi wamegeuka kuwa yatima. Wazazi wamepoteza watoto ni misiba kila mahali. Taasisi nyingi za Serikali kama shule na vituo vya afya miundombinu imeharibika. Barabara zimeharibika, madaraja yanachunguzwa nayo yanasemekana ni hatari kwa matumizi.

Wakati yote haya yakiendelea, kuna watu wanabuni kutapeli waathirika na walaaniwe. Natoa rai kwa Serikali hasa vyombo vya dola vishughulike na majambazi hawa kuanzia benki, maofisa wa benki iliyohusika kufungua akaunti hii. Na kama inawezekana hiyo benki iliyohusika ifungiwe hata kwa mwaka mmoja, kama adhabau ili iwe fundisho kwa benki nyingine.

Magufuli alipowateua watu wa kumsaidia katika Serikali yake, alilihutubia taifa na kuwaelezea Watanzania kwamba aliowateua alikuwa anawaamini.

Inasikitisha sana kuona watu walioaminiwa kumsaidia rais, wanatumia nyadhifa zao kwa kutumia udhaifu na matatizo ya wahanga kutaka kujinufaisha na ninaamini hata familia zao huko walikotoka zinasikitika.

Aidha, kama hawa watendaji waliotumbuliwa wameshindwa kuficha tamaa zao za kifisadi muda mfupi baada ya kupewa dhamana ya kuisaidia Serikali ya awamu ya tano, navishauri vyombo na taasisi nyingine zinazohusiana na uteuzi wa wasaidizi wa rais kuwa makini katika kuwapata wasaidizi wenye utu na uadilifu wa hali ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles