Na Renatha Kipaka
MKUU wa Mkoa wa Kagera, Meja Generali Mstaafu, Salim Kijuu aliagiza wafugaji wanaotumia mapori ya akiba kwa ajili ya malisho ya mifugo wawe wameondoka katika mapori hayo vinginevyo nguvu ya sheria itachukuliwa dhidi yao.
Alitoa agizo hilo jana alipozungumza na waandishi wa habari.
RC alisema kutokana na uharibifu mkubwa ambao umekuwa ukifanyika katika mapori hayo ametoa siku tatu kwa wafugaji wanaotumia mapori kuondoka.
Alisema hivi karibuni alitembelea mapori ya Biharamulo, Nyantakara, Burigi na Ruiga na kujionea hali halisi ya uharibifu wa hifadhi hizo.
RC alisema uharibifu huo ulitokana na shughuli za binadamu na uchungaji wa mifugo.
Alisema uharibifu unaofanyika katika hifadhi hizo ni ukataji wa miti ovyo, shughuli za kilimo ndani ya misitu na kwenye vyanzo vya maji.
Jenerali Kijuu alisema makundi ya wanyamapori yanatishiwa kutoweka pamoja na uoto wa asili.
Alisema kwa sasa wanyamapori wamechanganyikana na makundi ya n'gombe jambo ambalo linasababisha wanyama pori kuhama kutoka katika makazi yao ya asili na kuvamia makazi ya wananchi.
“Niseme tu nguvu hii siyo nguvu ya soda. Yeyote atakayekaidi agizo hili la kuondoka ndani ya siku tatu atataifishiwa mifugo yake,”alisema.
Alisema kutokana na mvua inayoenderea kunyesha, wananchi hawana budi watumie frusa hiyo kulima mazao ya chakula ili kuwa na akiba ya chakula.