30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

RC AAGIZA MAGARI MABOVU YASIRUHUSIWE BARABARANI

 

Na Tiganya Vincent

SERIKALI mkoani Tabora imeliagiza jeshi la polisi   kuendesha   ukaguzi wa magari yote yanayotoa huduma za usafirishaji wa abiria   kuhakikisha   mabovu yanazuiwa kutoa huduma hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa   wilayani Sikonge baada ya  ajali mbili za basi la Kampuni ya Adventure iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na la Kampuni ya HBS.  Ajali hizo zilitokea hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema hatua hiyo itasaidiz kuzuia ajali zinazototokea kutokana na ubovu wa vyombo hivyo.

Alisema   baada ya kuangalia gari la HBS  namba T960 AHH, bodi yake  ilionekana imechakaa ingawa lilikuwa linaendelea kutoa huduma ya usafiri.

Alimwagiza Kamanda wa Polisi Usalama wa Barabarani Mkoa wa Tabora (RTO)  kuanza mara moja ukaguzi wa magari yote ya abiria kila siku.

Mwanri alisema haiwezekani magari mabovu yaendelee kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na kuendelea kuhatarisha  maisha ya watu.

Alisisitiza kuwa gari lisiruhusiwe kusafiri likiwa bovu hadi   litakapofanyiwa maboresho ya kuondoa ubovu huo.

Ilielezwa kuwa  ajali ya basi la HBS ilisababishwa na uzembe wa dereva   ambaye alijaribu kulipita gari jingine katika upande usioruhusiwa na kujikuta akiingia katika daraja  na basi kupinduka.

Tukio hilo lilisababisha abiria  zaidi ya 20 kujeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sikonge.

Mmoja wa majeruhi wa gari hilo,   Sada Shabani alikiri dereva wa gari lao hakuwa makini   alipokuwa anapishana na gari jingine na kujikuta akiingia katika daraja,

Alisema   ajali hiyo ingeweza kuepukika kama dereva huyo angesubiri lori la mafuta lipite na yeye   aendelee na safari yake.

Wakati huohuo, Mwanri  aliagiza jeshi la polisi kuwatafuta madereva wa mabasi yote mawili waliosababisha ajali na kukimbia ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles