28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Raza aibukia suala la Escrow

Na Patricia Kimelemeta

MJUMBE wa Baraza la Wawakilishi na Mbunge wa Uzini, Zanzibar, Mohamed Raza, amesema ataishauri Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUKI), kuwaandikia barua wahisani ili kuwaeleza namna sakata la Tegeta Escrow lisivyowahusu Wazanzibari.
Alisema amefikia uamuzi huo ili kushawishi wahisani waendelee kutoa misaada yao kama kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Raza alisema sakata hilo limewaathiri wananchi wa Zanzibar kutokana na kunyimwa misaada na wahisani.
Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wanapaswa kuwaandikia barua wahisani na kuwaeleza ukweli.

“Sakata la Tegeta Escrow limewaathiri Wazanzibari kwa kunyimwa misaada wakati hawahusiki…hakuna kiongozi hata mmoja aliyetajwa kwenye kashfa hii.

“Nitalizungumza hili kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi ili viongozi wetu waweze kuwaandikia barua wahisani ya kuwaelezea jambo ambalo linaweza kusaidia kupata misaada,” alisema Raza.

Alisema kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, Serikali imeshindwa kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoahidi katika awamu iliyopita, hali ambayo inaweza kusababisha kukwamisha maendeleo.
“Mwaka 1995 wakati wa uongozi wa Rais mstaafu Dk. Salmin Amour (Komandoo), wahisani walitunyima misaada kwa madai ya kuwapo kwa migongano, lakini Tanzania ilishindwa kututetea badala yake walituambia hawawezi kutusaidia kwa sababu wahisani walikataa,” alisema.
Akizungumzia suala la rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Raza alisema kuna baadhi ya viongozi wa chama hicho kutoka Bara wanapita kwa wanachama wao na kutoa rushwa ili waweze kuchaguliwa kuwania urais.

“Ninawaambia wanachama wa CCM wachukue fedha zao, lakini wasiwachague kwenye mkutano mkuu,” alisema.

Alisema wananchi ndio wenye mamlaka ya kuwachagua viongozi wao siyo wana CCM peke yake.
Kuhusu utawala wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Raza alisema amejitahidi kuleta maendeleo na kwamba anapaswa kuongezewa muda ili amalizie alipoishia.
“Ningekuwa na uwezo ningemwambia Dk. Shein aendelee na awamu nyingine ili amalizie utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyoanzisha,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles