27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge: Usipodanganya hupewi kura

natseNa Khamis Mkotya, Dodoma

MBUNGE wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), amesema itachukua muda mrefu Tanzania kupata viongozi makini wanaojitambua, kwa sababu wananchi wengi hawana elimu ya uraia.
Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Bunge mjini hapa, Natse alisema katika mazingira ya sasa ni vigumu mgombea wa nafasi yoyote kupewa kura bila kudanganya.
Alisema katika hali hiyo, wananchi wengi wanashindwa kutofautisha majukumu ya mbunge na yale ya Serikali, hivyo inakuwa rahisi kuwadanganya.
“Usipowadanganya wananchi hawakuchagui, hii ndiyo hali halisi ya siasa Tanzania, utakuta mwanasiasa anaahidi vitu vikubwa ambavyo hawezi kutekeleza, huyo anapata sifa.
“Utakuta mtu anasema atajenga zahanati, mara atajenga barabara lakini wananchi hawamuulizi fedha atapata wapi, hapo wanapiga makofi na kushangilia.
“Hakuna mtu binafsi atakayeweza kujenga shule, zahanati wala barabara, hayo ni majukumu ya Serikali. Wananchi wetu bado hawatofautishi majukumu ya mbunge na ya Serikali,” alisema.
Alisema wabunge wengi watapoteza nafasi zao katika uchaguzi wa mwaka huu na kueleza kuwa wengi wao wataponzwa na ahadi nyingi walizotoa mwaka 2010.
Alikosoa hatua ya baadhi ya wabunge wanaokimbia majimboni katika kipindi hiki na kushindwa kuhudhuria mkutano wa Bunge la bajeti unaoendelea hivi sasa.
Aliwataka wananchi kuwakataa wabunge ambao katika kipindi hiki wanajifanya ni wakarimu na kuwa karibu na mazingira ya jimbo, akisema kuwa hawafai.
“Mbunge ambaye hakufanya kazi katika kipindi cha miaka mitano anakuja kufanya mwishoni hafai kwa sababu hana nia njema na wananchi isipokuwa dhamira yake ni kuwalaghai.
Katika hatua nyingine, Natse alijigamba katika uchaguzi wa mwaka huu, chama chake kitashinda Jimbo la Karatu kama ilivyo kawaida na kusema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kisahau ndoto za kutaka kulirejesha jimbo hilo mikononi mwao.
Alisema Karatu ni ngome ya Chadema isiyotetereka na kueleza kuwa chama chake kimeweka historia kubwa ya maendeleo ambayo wananchi wa Karatu hawawezi kuisahau.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles