27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk Hosea: Uchunguzi Escrow palepale

Edward Hosea mkuu wa TAKUKURUNa Debora Sanja, Dodoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema uchunguzi dhidi ya vigogo wa kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow unaendelea.
Kauli hiyo ilitolewa Dodoma jana na Mkurugenzi wa Takukuru, Dk . Edward Hosea alipokuwa akijibu maswali ya wabunge waliohudhuria semina ya Chama Cha Wabunge Wanaopambana na Rushwa (APNAC).
Kauli ya Dk. Hosea ilitokana na swali la Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), aliyetaka kujua kama taasisi hiyo ilishiriki kwa namna moja au nyingine kuwasafisha watuhumiwa wa Escrow.
Sendeka alihoji ni kwa vipi taasisi nyingine (Ikulu), inawasafisha watuhumiwa wa kashfa hiyo wakati Takukuru inaendelea na uchunguzi wake kitendo ambacho kinaweza kuharibu uchunguzi.
“Au kwa kuwa Takukuru na nyie mpo ofisi moja Ikulu mliwasiliana kuwasafisha watuhumiwa hao? Kama hamkushiriki kuwasafisha mseme Bunge hili kabla halijamaliza muda wake liwasaidie,”alisema Ole Sendeka.
Akijibu swali hilo, Dk. Hosea alisema taasisi yake haijamsafisha yeyote na bado inaendelea na uchunguzi wake.
“Sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria siyo kwa maelekezo kutoka kwa mtu yeyote… waliofikishwa mahakamani hatuwezi kuwasafisha na wale ambao bado uchunguzi unaendelea,”alisema.
Alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue aliwasafisha watuhumiwa hao katika eneo lake na kwamba Takukuru inaangalia eneo lake.
Itakumbukwa hivi karibuni, Sefue alisema imebainika aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yake, wote hawana hatia.
Rushwa kwa mitandao
Dk.Hosea pia alitoa onyo kwa wagombea wakiwamo wa nafasi za ubunge waliojiandaa kutoa rushwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kutuma fedha kupitia mitandao za kiganjani.
“Kwa sasa, Serikali imetuwezesha kudhibiti rushwa kwa njia ya mtandao, tunaye mtaalamu ambaye amesomeshwa kwa ajili hiyo, tunayo mitambo ya kisasa.
“Nawaambia wale waliojipanga mwaka huu kutoa rushwa kwa kutumia M-Pesa, Tigo- Pesa mwaka huu mjue mtaumia sana,”alisema.
Akizungumzia wagombea hasa wa nafasi ya urais ambao wameonyesha nia na baadhi wameanza kuchangia michango mbalimbali ikiwamo kwenye harambee, Dk.Hosea alisema kuwakamta watu hao inahitajika busara.
“Unapowakamata watu kama hao inabidi utumie ushahidi wa kutosha, hatumuogopi mtu, hata hivyo suala la uchaguzi ni nyeti na linasimamiwa na vyombo vingine pia,”alisema.
Aliwataka wabunge wenye malalamiko ya watu wanaotoa rushwa kwa wananchi kwenye majimbo yao wawasiliane na ofisi yake.
Alisema kwa wale wabunge wa majimbo wanaruhusiwa kutoa misaada ya maendeleo kwa wananchi wao, lakini kwa mujibu wa Sheria ya Gharama ya Uchaguzi, hairuhusiwi kutoa misaada hiyo kwa mtu mmoja mmoja.
Baadhi ya wabunge walilalamikia baadhi ya walioonyesha nia ya kugombea katika majimbo yao wakisema wanajipitisha na kugawa vitu mbalimbali kwa wananchi.
Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM) alitaka kujua nafasi ya Takukuru kwa Watanzania walioonyesha nia ya kugombea ambao wengine wameanza kuendesha harambee na kutoa misaada kanisani na misikitini.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy, (CCM) alitaka kujua jinsi Takukuru inavyoshughulikia rushwa ya ngono na rushwa kwa njia ya mtandao.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) aliitaka taasisi hiyo iwashughulikie wabunge wanaotoa misaada ya fedha nyingi katika majimbo yao tofauti na kipato chao.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), alihoji kama taasisi hiyo ilishawahi kumkuta na hatia mgombea yeyote kwa kutumia Sheria ya Gharama ya Uchaguzi.
Alitaka pia kujua kama Takukuru ina uwezo wa kumuondoa mgombea wa urais hasa CCM iwapo atathibitika katoa rushwa.
Awali akifungua semina hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika, aliitaka taasisi hiyo ianze kazi sasa isisubiri hadi Oktoba kwa kuwa majimboni tayari rushwa imeanza kutolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles