27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

RAYVANNY ATAWEZA MFUPA ULIOMSHINDA DIAMOND?

Na JOHANES RESPICHIUS

TUZO za Black Entertainment Television (BET) za nchini Marekani ni moja kati ya tuzo ambazo zinazofuatiliwa na watu wengi ulimwenguni.

Tuzo hizi zimejipatia umaarufu mkubwa hasa kutokana na kuwa tuzo ambazo zimekuwa zikiwashirikisha wasanii mbalimbali kutoka mabara tofauti.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo wasanii wake wamekuwa wakitajwa kuwania tuzo hizo katika kipengele kilichowekwa hivi karibuni mahususi kwa ajili ya wasanii kutoka Afrika cha Best International Act Africa.

Mwaka jana, staa wa muziki wa Bongo Fleva na mmiliki wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alitajwa katika kipengele hicho hicho  akichuana na mastaa wengine wa Afrika wakiwamo Wizkid, Yemi Alade wa Nigeria, AKA, Cassper Nyovest na Black Koffie wa Afrika Kusini.

Tuzo hiyo ilikwenda kwa prodyuza, Dj na mwimbaji mwenye mafanikio makubwa katika muziki nchini Afrika Kusini, Black Koffie. Tanzania haijawahi kutwaa tuzo hiyo tangu kuanzishwa kwake.

Mashabiki wengi wa Diamond walikuwa na matumaini makubwa kwamba staa hiyo angerudi na tuzo hiyo kutokana na kiwango ambacho alikuwa tayari amefikia katika kuliteka soko la muziki la hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

Lakini mambo yalikuwa ndivyo sivyo na mwisho wa siku tuzo hiyo ikanyakuliwa na Koffie, staa ambaye kwa hapa nchini hakufahamika kivile na hata nje hakupewa nafasi kubwa ya kushinda.

Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Juni 25, mwaka huu  katika Ukumbi wa Microsoft Theater mjini Los Angeles, Marekani zikiwa zimewashirikisha mastaa wakubwa ulimwenguni.

Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla imepata bahati ya kuwakilishwa na msanii chipukizi kutoka WCB, Raymond ‘Rayvan’ na kuwa msanii pekee wa Bongo Flava aliyechaguliwa kuwakilishi katika tuzo hizo.

Rayvanny amechaguliwa katika kipengele cha International Viewer’s Choice Awards ambacho sharti lake lazima upigiwe kura nyingi na mashabiki ndipo ushinde tuzo hiyo.

Kipengele hicho kinawaniwa na wasanii wengine kama Dave wa Uingereza, Amanda Black (Afrika Kusini), Changmo (Korea Kusini), Daniel Caesar, Remi na Skip Marley wote wa Jamaica. Mwaka jana tuzo hiyo ilikwenda kwa Falz wa Nigeria.

Ni dhahiri kwamba Rayvanny ndiye msanii anayechipukia anayeangaliwa zaidi na vyombo vingi vya habari Afrika kutokana na utunzi na uimbaji wake ambapo licha ya kuwa na nyimbo chache tayari amekwishatajwa katika tuzo za kimataifa kama vile tuzo za Afrika Entertainment Awards, USA.

Macho ya wengi yapo kwa Rayvanny yakiangalia kama ataweza kutwaa ufalme wa kuwa Mtanzania wa kwanza kuchukua tuzo ya BET.

Lakini cha muhimu tunapaswa kuangalia kilichomkwamisha Diamond kuchukua tuzo hiyo na  kufanya marekebisho yatakayomwezesha Rayvanny kushinda kiulaini.

Kwa kuwa kigezo kikuu cha kutwaa tuzo hii ni kupigiwa kura, Watanzania wenyewe ndiyo wenye uwezo wa kumfanya achomoke na tuzo hiyo au lah!

Suala hili naamini mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva na wadau kwa ujumla watasahau timu zao na kuweka utaifa mbele na kumuunga mkono Rayvanny ili afanikiwe kuchukua tuzo hiyo kubwa.

Misimu iliyopita katika tuzo kama hizi ambazo amekuwa akishiriki Diamond au hasimu wake, Ali Kiba mashabiki wamekuwa wakiweka timu mbele hivyo kujikuta wakimpigia kura mpinzani wa msanii ambaye si wa timu yake ili kumkosesha ushindi, jambo ambalo lilikuwa likisababisha taifa kujikuta linaondoka mikono mitupu.

Hali hii ndiyo imekuwa ikidhoofisha afya ya muziki wetu.  Ni wakati wa kujifunza kutokana na makosa ambayo yamekuwa yakifanyika na badala yake kumpigia kura kwa wingi Rayvanny ili kuitambulisha vyema Tanzania.

Haya sasa wadau wa muziki wa Bongo Fleva, kazi ni kwenu sasa kumsapoti Rayvanny kwa kumpigia kura nyingi ili aweze kuchomoka na ushindi.

Tukumbuke kwamba, ushindi wake ni ushindi wa Tanzania kwa ujumla wake. Yeye anakwenda kushiriki, lakini ni kwa niaba ya Watanzania wote. Tumpigieni kura kwa wingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles