22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

MAMBO 20 YA KUZINGATIA UKIWA KIJANA – 5

Na ATHUMANI MOHAMED

TUNAENDELEA na somo letu ambalo ni muhimu sana kwa kijana yeyote mwenye nia ya kuwa tajiri au mwenye mafanikio baadaye.

Kama nilivyoeleza awali yapo mambo mengi sana ya muhimu ya kuzingatia ili kutengeneza mazingira ya kuwa na maisha bora hapo baadaye. Hata hivyo katika mada hii nimekumegea yale ya muhimu zaidi 20.

Katika matoleo ya mwanzo, tayari tumeshaona mambo 11 na leo tunaendelea na jambo la 12 na kuendelea.

  1. JIENDELEZE KIELIMU

Ni kweli kufaulu shule siyo kufaulu maisha na kadhalika kufeli shule siyo kufeli maisha, lakini elimu inatajwa kama sehemu ya msingi ya mafanikio ya binadamu.

Ukiwa na elimu ya kutosha hakuna kitu cha kukubabaisha mbele ya safari. Pima elimu uliyonayo, ikiwa unaona upo katika kiwango cha chini, jiendeleze.

Mfumo wa elimu siku hizi karibu ulimwenguni mwote ni rafiki. Unaweza kuendelea kufanya kazi huku ukitimiza malengo yako kielimu.

Soma. Tafuta kozi au ngazi ambayo hujafika ili kujiongezea maarifa. Inawezekana una elimu ya darasa la saba tu. Isikukatishe tamaa, jiunge hata na masomo ya QT ambayo yatakuwezesha kuhitimu elimu ya kidato cha nne kwa miaka miwili.

Mwanzo huo unaweza kukupaisha mbali zaidi  kielimu. Ni wazi kuwa baadaye utakuwa na miradi mingi, sasa ili uweze kuisimamia vizuri ni sahihi zaidi kuwa na elimu ya kutosha.

Kusoma hakuna mwisho, lakini zaidi unaweza kuwa msomaji mzuri wa vitabu kwa kadiri uwezavyo. Kuna siri kubwa sana katika kujisomea. Ukiweza hilo, maisha yako yatakuwa rahisi.

Unaweza kupoteza vitu vingi vya kushikika, lakini siyo rahisi kupoteza wala kuibiwa hazina ya elimu utakayokuwa umeihifadhi kichwani mwako.

  1. SAIDIA WENGINE

Bila kujali uwezo wako, jenga tabia ya kuwasaidia wahitaji. Muhimu kwako ni kuangalia wale ambao kweli ni wahitaji, wenye dhiki.

Msaada wako wa mlo mmoja kwa mtu mwenye uhitaji una thamani kubwa sana kwa Mungu. Kumbuka kwamba mafanikio yetu yana uhusiano mkubwa na namna tunavyotumika kuwasaidia wengine.

Mungu huwakumbuka wale ambao hukumbuka kuwasaidia wenzao wanaowaona wana uhitaji. Kulingana na uwezo wako, kuwa msaada kwa wengine. Wape faraja wagonjwa, wafiwa n.k na utashangaa namna milango yako ya mafanikio itavyofunguka.

 

  1. TOA ZAKA

Hii ni kanuni ya kiimani ambayo ina uhusiano mkubwa sana kwenye mafanikio. Tafuta elimu ya kidini na uelewe sawasawa namna inavyokupasa kutoa zaka/sadaka kwa kiwango kilichoelekezwa kisha timiza hilo.

Ukiwa mwaminifu kwenye kutoa zaka na maisha yako yote ukajiwekea utaratibu wa kutoa zaka, mafanikio kwako halitakuwa jambo la kusimuliwa.

  1. WEKA AKIBA

Kuweka akiba ni miongoni mwa kanuni kuu za mtu anayesaka mafanikio. Achana na tabia ya kuishi kwa mazoea. Usiwe na tabia ya kula zote unazopata leo ukiwa na matumaini ya kupata kesho.

Hakuna anayeijua kesho yake. Jifunze kuweka akiba. Hii haina tofauti kubwa sana na kuwekeza ambapo nilikuelezea huko nyuma lakini hapa ni kwamba unahifadhi fedha.

Utaratibu mzuri uliopendekezwa na wataalamu wa uhamasishaji mafanikio ni kuangalia kipato chako, kiwe kwa siku, wiki au mwezi, kisha gawa mara mbili. Nusu ya kwanza weka akiba benki. Nusu nyingine igawe mara mbili, nusu moja ifanye kwa matumizi ya chakula, kisha nyingine inayobaki iweke akiba ndogo kama dharura.

Utaratibu huu ni mzuri na unaweka nidhamu nzuri ya fedha. Mafanikio ya utaratibu huu ni makubwa kwa sababu kwanza, ile akiba kuu unayoweka benki huwa na riba baada ya muda fulani.

Ni kweli kwamba ni kanuni ngumu, inayowashinda wengi lakini waliofanikiwa kumudu hili hasa kuanzia kipindi cha ujana wao, wamefanikiwa baada ya muda mfupi sana.

Jumamosi ijayo tutamalizia sehemu ya mwisho, kuna mambo ya msingi zaidi ambayo yatakamilisha mada hii.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles