25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ray C aliza watu

Ray-C

*Akamatwa usiku akiwa hoi kwa kilevi

*Jitihada za Kikwete, Ruge zawa kazi bure

 

NA AGATHA CHARLES

MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila maarufu kwa jina Ray C, jana alizua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kusambazwa kwa video iliyokuwa ikimuonyesha yuko ndani ya gari la polisi huku amelewa chakari.

Video hiyo ilisambazwa katika mitandao ya kijamii ya Whatsapp, Instagram na Jamii Forum ikimuonyesha akiwa ndani ya gari la polisi huku akijibizana nao pamoja na watu waliokuwa eneo hilo.

Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata awali na baadaye kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime, zilieleza kuwa Ray C aliokotwa na wasamaria wema maeneo ya Facebook, Kinondoni, saa 5 usiku akiwa ameshika kisu ambacho alitaka kukitumia kujidhuru.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alilieleza MTANZANIA Jumamosi kuwa msanii huyo alichukua kisu kwa nia ya kujichoma mwilini na wakati polisi wanafika eneo hilo tayari alikuwa amekwishajijeruhi baadhi ya sehemu za mwili wake.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Fuime alisema Ray C alikutwa na polisi waliokuwa doria saa 5 usiku akiwa katika mazingira ya kujiumiza mwili wake huku tayari akiwa amejijeruhi baadhi ya sehemu za mwili wake.

“Ray C, jana usiku askari walimkuta katika mazingira ya kujiumiza na alitaka kujiua na tayari alikuwa na majeraha kidogo mwilini hivyo alipelekwa hospitali na polisi.

“Lakini hayuko chini ya ulinzi, si kila jambo lenye asili ya jinai tunachukua hatua, alikuwa amelewa, alikamatwa katika mazingira ya ulevi angekuwa ‘sober’ hapo sawa. Tulichokifanya ni kumsaidia na kumwacha hospitali aendelee na matibabu,” alisema Kamanda Fuime.

Alipoulizwa Mratibu wa Tiba wa Hospitali ya Mwananyamala, Nkungu Daniel ambako Ray C alipelekwa kwa matibabu kuhusu aina ya kilevi ambacho msanii huyo aligundulika kukitumia alisema hilo hawezi kulizungumzia kwa sababu maadili ya kazi yake hayamruhusu kutoa siri za mgonjwa.

“Alifikishwa hapa usiku, akahudumiwa na kuruhusiwa usiku huo huo ambao ni sawa na asubuhi ya leo,” alisema Dk. Daniel.

Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka Hospitali ya Mwananyamala ambako huwa anahudhuria kliniki ya tiba ya watu walioathirika na dawa za kulevya, zilieleza kuwa mahudhurio yake kwa ajili ya kutumia dawa aina ya methadone inayotoa sumu inayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya mwilini si mazuri kwa sasa.

“Mahudhurio yake si mazuri, kuna wakati namwona anakuja na wakati mwingine anaweza kukaa muda hivi hajaja,” alisema mmoja wa matabibu katika kliniki hiyo.

Katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Ray C anaonekana akiwa ndani ya gari huku akishindwa kuwatambua watu waliokuwa wakimsaidia na yanasikika majibizano ya maneno baina yake na watu hao. Majibazano hayo yalisikika hivi;

“Kuwa serious, shika na simu.. Mama yangu…sasa utampa msaada eeeh,..poa usijali dada yangu huyu sema hajanifahamu vizuri, kitambo sana… atanipaje msaada, nawapenda jamani…lakini mbona huelewi, acha madawaaaa, tulia..achia, achiaaa.…tulia..acha madawa….eeh jamani, eeh jamani, jamani nakufa…jamani natekwa wahuni wote hao.. sogea…dada Rehema hutekwi na mtu.. nimetekwa.”

Watu mbalimbali walioiona video hiyo wametoa maoni  na waliomshuhudia wakati akichukuliwa na polisi kupelekwa hospitalini nao walieleza jinsi walivyoumizwa na kubadilika kwa mwenendo wa msanii huyo baada ya kupata msaada wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete wa kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni msanii wa filamu, Esha Buheti, aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Instagram akiwaeleza kuwa:

“Nashindwa hata niongee nini jamani, Ray C, leo Kinondoni umenitoa machozi, jamani tufanye kitu tumsaidie Ray C, I mean it, jamani siku zote nilikuwa najua anaonewa ila nilichokishuhudia leo nimeumia kutoka moyoni amedhalilika mwanamke mwenzetu, jamani tufanyeje?

“Nilikuwa na Kabula Kinondoni kwa Wapemba tumefuata chips mara tukasikia mtu anasema mie Ray C nataka kuvua nguoo, nikajua utani kushuka ni Ray C anasema nishikeni kuna watu wanataka kuniteka, alikuwa na nguvu sana watu kumshika akaanza kuongea vitu havieleweki, akaanza kutafuta kisu ajichome.

“Watu walimzuia sana walishindwa, akaanza kugaragara kwenye matope akipiga kelele, kiukweli nilijikuta nalia mara ikaja gari ya polisi ikambeba ila kwa tabu sana, alikuwa akipiga kelele jamani nisaidieni msiniache. Mpaka anaondoka na polisi sikujua anapelekwa wapi, alikuwa kama mtu aliyepata kichaa.”

Wasanii mbalimbali na mabloga nao waliandika katika akaunti zao wakiunga mkono hoja ya kumsaidia Ray C.

Desemba 2012, Ray C na mama yake, Margareth Mtweve, walikwenda Ikulu kumshukuru Rais mstaafu Kikwete kwa kumsaidia msanii huyo kuachana na unga na kuanza kliniki ya kupata dawa za methadone.

Taarifa zilidai Mkurugenzi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba, alikabidhiwa Ray C amsimamie katika kazi zake na 2014 alianzisha taasisi ya Ray C foundation kwa ajili ya kuelimisha madhara ya dawa za kulevya kwa vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles