KINDA wa timu ya Manchester United, Marcus Rashford, amepoteza nafasi yake katika kikosi cha timu ya Taifa ya England baada ya kuondolewa kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester United.
Uamuzi huo ulifanyika tangu ujio wa kocha mpya wa Manchester United, Jose Mourinho, ambaye aliamua kumtumia zaidi Zlatan Ibrahimovic kama mshambuliaji wake tegemeo katika michezo ya Ligi Kuu England.
Rashford ametupwa hadi kikosi cha vijana cha timu ya taifa chini ya umri wa miaka 21, baada ya Kocha wa England, Sam Allardyce, kuthibitisha kwamba hana nafasi kwa chipukizi huyo kuelekea katika mchezo dhidi ya Slovakia wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia.
Msimu uliopita Rashford alifanikiwa kushinda mabao nane katika michezo 18 ya ligi kuu ambapo baadaye Kocha wa zamani wa timu ya taifa, Roy Hodgson, alimuita kuongeza nguvu katika michuano ya Euro 2016.
Kitendo cha kufukuzwa kwa Louis van Gaal na kuteuliwa Mourinho kuwa kocha mkuu wa Manchester United kiliondoa uhakika wa kinda huyo kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.