31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Kama si TFF, Simba, Yanga tungeziona Chamazi

SIMBA, YANGANa ABDUCADO EMMANUEL-DAR ES SALAAM

MOJA kati ya timu zenye viwanja vidogo nchini England ni Shrewsbury Town, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (League One).

Licha ya udogo wa uwanja wake wa Greenhous Meadow unaochukua watazamaji 9,875, bado haikuondoa haki yao ya kupambana na Chelsea katika uwanja wake wa nyumbani katika mchezo wa raundi ya nne ya michuano ya kuwania taji la Capital One Oktoba 28 mwaka juzi.

Hakuna asiyejua wingi wa mashabiki wa Chelsea, lakini miamba hiyo ililazimika kufunga safari hadi jijini Shrewsbury kucheza na timu hiyo, kutokana na Chama cha Soka England (FA) kuongoza soka lake kwa weledi mkubwa kwa misingi ya haki na usawa bila kupendelea baadhi ya timu.

Hata nchini Afrika Kusini, timu ya Bidvest Wits ni miongoni mwa timu zenye viwanja vidogo nchini humo unaoitwa Bidvest zamani Milpark, lakini linapokuja suala la mechi zake za nyumbani hupewa nafasi na Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA), kutumia uwanja wake wa nyumbani wenye uwezo wa kuchukua takribani mashabiki 5,000 tu.

Licha ya wingi wa mashabiki wa timu kongwe za huko, Kaizer Chiefs, Olando Pirates na Mamelodi Sundowns, lakini timu hizo hulazimika kuifuata Bidvest Wits pale wanapokuwa ugenini ili kuipa nafasi timu hiyo kufaidika na mashabiki wake kwenye uwanja wake wa nyumbani na huu mfumo ndio unaotumika na mashirikisho ya soka duniani kote.

Hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), linasisitiza uungwana kwenye mchezo huo (fair play), hutambua mfumo huo wa timu kucheza kwa mfumo wa nyumbani na ugenini (home and away).

Hapa nchini hali ni tofauti kwani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limekuwa likiminya uhuru wa timu kutumia viwanja vyake katika kucheza mechi zake za nyumbani. Wakidai kuwa eti kutokana na sababu za kiusalama kutokana na udogo wa baadhi ya viwanja.

Lakini TFF hufanya hayo yote kwa timu mbili za Simba na Yanga, ambazo ndizo timu pekee kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara zinazocheza mechi nyingi za nyumbani kuliko nyingine zote.

Mpaka sasa Yanga na Simba zimekuwa haziendi kucheza mechi zake za ligi na zile za Kombe la FA ugenini katika Uwanja wa Azam Complex, unaomilikiwa na mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Uwanja wa Mabatini (Ruvu Shooting, JKT Ruvu), Karume (African Lyon) na ule wa Manungu unomilikiwa na Mtibwa Sugar.

Mechi zote za ugenini zinazohusisha timu za Azam FC, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, African Lyon na timu zote nyingine za Dar es Salaam, Simba na Yanga hupata haki ya kuchezea kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Taifa.

Hata zile za Mtibwa Sugar zinazotakiwa zikachezwe Manungu, basi hulazimishwa zikapigiwe Jamhuri pale mjini Morogoro, pia wakienda kucheza na Mwadui, TFF huipanga mechi hiyo ikachezwe kule Kambarage badala ya ule wa Mwadui Complex unaomilikiwa na matajiri hao wa Shinyanga.

Kwenye Ligi Kuu England, Uwanja wa Vitality unaomilikiwa na Bournemouth, ndio mdogo kuliko wote kwa timu zote za ligi hiyo ukichukua watazamaji 11,464, lakini timu zote zitalazimika kwenda kucheza hapo zitakapocheza ugenini dhidi ya wenyeji hao.

Hata Manchester United yenye uwanja mkubwa kuliko timu za ligi hiyo unaoitwa Old Trafford unaochukua watazamaji 75,653, nayo italazimika kuifuata Bournemouth na kucheza katika uwanja huo mdogo, hii yote ni kufuata sheria zilizowekwa kiweledi na FA ili kuipa haki timu hiyo pamoja na mashabiki wake kuipa sapoti timu yao.

Kitakwimu Simba na Yanga zinatarajia kucheza mechi 20 kila mmoja zikiwa nyumbani ukijumlisha na mechi zao mbili za wenyewe kwa wenyewe huku mechi nane zikicheza ugenini na mbili katika viwanja huru.

Simba na Yanga kikawaida zilitakiwa kucheza mechi 15 tu za nyumbani, lakini kutokana na hali hiyo wameongezewa mechi nne nyingine za ziada za kuwa nyumbani, ambazo ni dhidi ya Azam FC, JKT Ruvu, Ruvu Shooting na African Lyon, huku wakibebwa tena kwa kucheza katika viwanja huru pale wanapokutana na Mwadui na Mtibwa Sugar.

CAF na Fifa kwa hapa Tanzania inavitambua viwanja vinne vyenye uwezo wa kuchezewa mechi za kimataifa zinazoandaliwa na mashirikisho hayo, ambavyo ni Taifa, Uhuru, Azam Complex unaochukua watazamaji 5,000 (vyote Dar es Salaam) na CCM Kirumba, Mwanza.

Ili viwanja vipewe hadhi hiyo, basi lazima viwe na sehemu nzuri ya kuchezea, uzio wa kutenganisha sehemu ya kuchezea na majukwaa ya mashabiki, vyumba vinavyokidhi vya kubadilishia nguo, ubao wa matokeo, chumba cha kupima wachezaji na chumba cha kukaa wasimamizi wa mchezo.

Uwanja wa Azam Complex, mpaka sasa umefikisha miaka mitatu tokea uanze kutumika kwenye mechi za kimataifa, lakini pia ni miaka mitano toka ufunguliwe rasmi kuchezea mechi za Ligi Kuu Agosti, 2011.

Kigezo cha usalama hakina mashiko kwa sasa, kwani tuliwahi kushuhudia Simba na Yanga zikitumia Uwanja wa Azam Complex kucheza baadhi ya mechi zake za ligi miaka minne iliyopita baada ya Uwanja wa Taifa kufungwa kutokana na kufanyiwa ukarabati maalumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles