30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS ZUMA HAKUPENDA RAMAPHOSA AMRITHI


Na BALINAGWE MWAMBUNGU

CHAMA kikongwe cha African National Congress (ANC) kimefanya Mkutano Mkuu wa 54 wiki iliyopita kumchagua Cyril Ramaphosa kuwa rais wake. Kuna mambo ambayo tunaweza kujifunza kutoka chama hicho kwake.

Moja, ni kitendo cha mfanyabiashara kuteuliwa kugombea nafasi ya juu katika chama. Rais wa ANC ndiye atakuwa mgombea wa nafasi ya Rais nchini Afrika Kusini mwaka 2019.

Pili, ni kuteua majina ya watu wenye mizizi na historia katika chama. Hapa kwetu jambo hili halipo kikatiba, lakini  wafanyabiashara wanaogopwa na wakishinda wanahisiwa kuwa wametumia utajiri wao ‘kuwanunua’ wapigakura.

Katika chaguzi za huko nyuma, wafanyabiashara wengi walipita na kugombea ubunge, kwa sababu ‘kununua’ wajumbe ilikuwa jambo la kawaida. Wagombea walikuwa wanatoa usafiri kwa wajumbe, wanawapatia posho, wanawapangia mahali pa siri pakulala na kuwapeleka kwenye ukumbi wa mkutano.

Baadaye likafanyika jaribio la kukataza kabisa kuwa mtu achague kimoja—biashara au siasa, lakini ikashindikana. Afrika Kusini, kama ilivyo Marekani, mfanyabiashara anaweza kuwa rais wa nchi mradi tu uwepo mwongozo wa kukataza—rais asijishughulishe na biashara zake akiwa madarakani.

Jambo la tatu, tumejifunza kwamba kumbe Rais aliyeko madarakani anaweza kutopenda kurithiwa na msaidizi wake mkuu — Makamu wa Rais.

Hapa nyumbani lilitokea kwa mara ya kwanza katika historia ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Rais Ali Hassan Mwinyi akiwa madarakani, hakuweza kuishawishi Halmashauri Kuu kumteua aliyekuwa Makamu wa Rais, kwa shinikizo la Rais Mstaafu, Mwalimu Julius Nyerere. Akatishia kujitoa CCM kama jina la John Malecela litakuwamo kwenye orodha ya wagombea.

Katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea urais, Rais Jakaya Kikwete, hakutumia ushawishi wake kwenye Kamati Kuu, ili jina la Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal liweze kuwamo katika majina matano yaliyopelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa uteuzi. Kamati Kuu ya CCM iliyatupa kapuni majina maarufu—likiwamo la aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda!

Mambo hayo yamejirudia huko Afrika Kusini, ambako Rais Jacob Zuma, hakupenda Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa, amrithi kiti cha urais wa ANC—badala yake akaelekeza nguvu zake kwa mtalaka wake—Nsozana Dlamini, kwa kuwa aliangalia masilahi yake binafsi badala ya masilahi mapana ya chama chake. Aliamini kwamba NDZ kama anavyoitwa, akipata nafasi ya urais wa chama, atakuwa amepata tiketi ya kugombe urais wa nchi katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2019. Rais Zuma aliamini kwamba NDZ angekuwa ngao yake akishaondoka madarakani kutokana na kashfa za rushwa zinazomkabili.

Wingi wa wajumbe wa mkutano mkuu wa ANC umetuonyesha kuwa, chama hicho kina wanachama wengi na kina mfumo mzuri wa uwakilishi, ingawaje kwa utaratibu wao, rais wa chama anaweza akaondolewa wakati wowote kwa sababu mbalimbali.

Mkutano Mkuu wa ANC ulikuwa na wajumbe 5,000 kutoka sehemu mbalimbali za Afrika Kusini. Wagombea wa nafasi ya rais walikuwa wengi na walizunguka majimboni kutafuta kuungwa mkono. Haikuwa rahisi kutabiri nani angechaguliwa kujaza nafasi hiyo aliyokuwa anaishika Zuma, ambaye muda wake wa miaka mitano wa kuongoza chama ulikuwa umekwisha.

ANC hakikubahatisha kuteua majina ya watu wawili—Nkosazana Dlamini na Cyril Ramaphosa. Wote wana mizizi na historia katika chama. Walishiriki vilivyo katika harakati za kupambana na udhalimu na ubaguzi wa rangi wakati wa utawala wa makaburu. Tofauti na hapa kwetu—watu wanaweza kuibuka tu wakati wa uchaguzi na kutaka kugombea nafasi mbalimbali—udiwani, ubunge na urais.

Nkosazana (68), ni mwanaharakati tangu enzi za ubaguzi wa rangi. Amekuwa waziri katika awamu zote za Nelson Mandela, Thabo Mbeki, Kgalema Motlnthe na Jacob Zuma na alikuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).

Cyril Ramaphosa (65), alishiriki katika harakati za ukombozi na ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, pia alikuwa Makamu wa Rais wa ANC na ni mfanyabiashara. Alikuwa mpigania haki za wafanyakazi wa sekta ya madini na ndiye aliongoza mazunguzo na makaburu ya kumtoa gerezani Nelson Mandela na kuleta utawala wa kidemokrasia.

Katika chama chochote cha siasa, makundi huwa hayaepukiki—kwa sababu kila mjumbe anakuwa na mtu wake. Hapa Tanzania kabla ya uchaguzi wa mwaka 2005, lilizaliwa kundi ndani ya CCM lililojiita wanamtandao na likafanikiwa kumweka madarakani ‘mtu wao’ kwa sababu walizozijua wao.

Katika uchaguzi uliomalizika mjini Dodoma hivi karibuni, ulikwenda sambamba na ule wa ANC uliofanyika jijini Johannesburg. Kulikuwa na mgombea moja tu wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli, tofauti na ANC ambacho kiliteua majina mawili kugombea nafasi ya urais wa chama. Katika mfumo wa kuwa na jina moja la mgombea, wajumbe hulazimika kupiga kura ya ‘Ndiyo’.

Uchaguzi wa ANC ulikuwa na ushindani mkubwa. Lakini pia wingi wa wajumbe wanaowakilisha sehemu mbalimbali na masilahi ya vikundi tofauti, ni nguzo mojawapo ya demokrasia shirikishi katika chama chochote cha umma (mass party). Unapokuwa na idadi ndogo ya wajumbe unaibana demokrasia, unapunguza ushiriki wa watu wengi kwenye masuala ya maamuzi mazito na hivyo kuwanyima watu ushiriki kwa njia ya uwakilishi.

Chama cha ANC kimepungua katika umaarufu na kutikiswa na kashfa za kuwalinda wala rushwa. Serikali chini ya uongozi wa Zuma, imepakwa matope ya rushwa na kutowajali watu wa hali ya chini. Kwa mtazamo watu wengi, walitaka ANC mpya.

Ingawaje ushindi wa Ramaphosa ni mwembamba, umepokelewa vizuri na wananchi, lakini kuna wanachama wa ANC ambao hawakuridhika na wamesema watakwenda mahakamani, kitu ambacho hapa kwetu hakijawahi kutokea kwa chama tawala.

Kama NDZ angechaguliwa, ANC kingeingia katika mgogoro mkubwa na labda ungekipasua chama. Kundi mojawapo la wanachama wa ANC liliamini kuwa ni mfano mbaya kwa watawala kupanga nani wa kumrithi—ni sawa na kuendeleza ufalme.

Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Ramaphosa, kama uteuzi wake hautatenguliwa na mahakama, atapata fursa ya kukiunganisha chama, ili kiingie kwa nguvu moja katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2019.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles