25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

BAADA YA MUGABE NANI ANAFUATA?


Na Ndahani  Mwenda

NCHI nyingi za Afrika zilipata uhuru kwenye miaka ya 1960. Nchi takribani 17 zilipata uhuru mwaka 1960, Tanzania ilipata uhuru  mwaka 1961 Uganda 1962 Kenya 1963 na Ghana 1957 na nyingine zilipata miaka 1970.

Zimbabwe, Afrika Kusini na Namibia ndiyo nchi zilizochelewa kupata uhuru kutoka kwa mkoloni. Na hii yote ni kutokana na mkoloni kuwekeza vilivyo katika nchi hizo, iliwawia vigumu sana kuondoka maana walikuwa na mali nyingi kama viwanda, mashamba na migodi.

Baada ya uhuru nchi nyingi za Afrika zilipitia nyakati za hatari hasa kipindi cha wimbi la kuwapindua viongozi, Rais wa Tanganyika enzi hizo Julius Nyerere alinusurika kupinduliwa.

Baada ya hapo Nyerere alilifanyia marekebisho jeshi alilolirithi kutoka kwa mkoloni mwaka 1964 ndipo likazaliwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Nyerere akaponea hapo.

Miaka miwili baadaye aliyekuwa rafiki yake Rais wa Ghana Kwame Nkurumah akiwa kwenye matibabu iliyokuwa Soviet (USSR) jeshi la nchi yake likatangaza kumpindua.

Hilo wimbi liliendelea kusambaa Afrika, nchi zilizokubwa ni pamoja na Tunisia, Togo, Nigeria, Misri, Algeria, Benin, Guinea Bissau, Guinea ya Ikweta. Hiyo yote ilisababishwa na watawala kuwasahau katika ufalme wa mbigu maveterani wa vita katika ukombozi kutoka kwa mabeberu.

Kabla ya Joseph Arthur Ankrah hajampindua Kwame Nkurumah  Februari 24,1966, Misri ndiyo nchi ya kwanza kutokea mapinduzi ya Kijeshi Barani Afrika. Muhammad Naguib alimpindua Mfalme Farouk mwaka 1952 kabla ya yeye kupinduliwa na Gamal Abdel Nasser mnamo 27 Februari 1954.

Muasisi wa Taifa la Algeria Ahmed Ben Bella naye alipinduliwa. Kama nilivyoeleza hapo juu nchi nyingi za Afrika zilipitia mapinduzi ya kijeshi mara baada ya kupata uhuru.

Tokea hapo demokrasia ya Afrika imekuwa ya kutilia mashaka, kwani hata wale waliopindua nao walipinduliwa na hata walioingia kwa sanduku la kura za wananchi wamekuwa waking’ang’ania madarakani. Kuna wale waliopindua halafu wakadumu mpaka leo hii.

Mwaka 1979 Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema Mbasogo aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi, mpaka leo bado ni Rais wa nchi hiyo, amegoma kuacha ngazi licha ya kutawala kwa miaka 38!

Mbasogo amegeuza nchi ni mali yake, amempa mwanae wa kiume umakamu wa Rais, kijana anatumia fedha za umma vibaya, ananunua magari na majumba ya gharama kubwa huko Ulaya mpaka Serikali za huko zimeanza kuchunguza mali zake. Hilo ndilo tatizo la viongozi wengi wa Afrika, huwa wakiingia madarakani wanajisahau Kabisa.

Hata huku Afrika Mashariki tunao, kina Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu Januari 29, 1986 mpaka leo hii (miaka 31) hataki kuondoka. Mkewe ndiye Waziri wa Elimu, mwanae wa kiume Muhoozi Kainerugaba ana cheo kikubwa jeshini, na inasemekana anamuandaa aje kumrithi!

Yoweri wa miaka 1990 si huyu wa miaka ya 2000 ama miaka 2010. Amebadilika! hapo awali wakati anaingia madarakani alisifika kwa utawala wa demokrasia, ikaaminika ni mtawala mzuri, akandika na vitabu  kama ‘What is Africa problem’  (1992) na kile cha ‘ Sowing the Mustard Seed, (1997) vyote hivyo alikuwa akilaumu watawala wa Afrika, lakini leo anaishi yale aliyokuwa akiyapinga. Nasikia kitabu chake cha Sowing the Mustard Seed amekifanyia uhariri na kuondoa maneno yote aliyokuwa akimsifu aliyekuwa rafiki yake mkubwa na mshirika wake wakati wakiwa mstini wakisaka madaraka Kiiza Besigye.

Yoweri Museveni amediriki kuweka msukumo ili Katiba ya Uganda ichezewe kwa kuondoa kipengele cha ukomo wa umri kwa mgombea Urais. Kwa sasa Museveni ana miaka 73, na Katiba ya Uganda Ibara 116 inataka mgombea asizidi miaka 75. Kwa hiyo Museveni anataka kugombea mwaka 2021. Kweli madaraka yanalevya!

Kwa kuwa viongozi wa Afrika wana ‘kaugonjwa ka kuambukiza’ka-uchu wa madaraka baada ya Museveni kuchezea katiba  nani atafuata?

Bila shaka hilo ni swali linalogonga vichwa vya wengi. Ukiachana na Museveni kuna marais wengi wa Afrika wamekaa madarakani muda mrefu

Yafahamu majina na muda waliokaa madarakani katika mabano. Teodoro Nguema – Guinea ya Ikweta (38) Robert  Mugabe – Zimbabwe (37), Paul Kagame- Rwanda (17) Pierre Nkurunziza – Burundi (12), Joseph Kabila – DRC (16), Eduardo Dos Santos-Angola (37). Dos Santos ameng’atuka Agosti mwaka huu.

Waliofia madarakani au kuondolewa kwa nguvu kuanzia mwaka 2009-2017, ni  Omar Bongo Ondimba alitawala Gabon kwa miaka 42 akafia madarakini mwaka 2009, Muamar Gaddafi alikaa madaraka tangu mwaka 1976-2011 alipopinduliwa, Hosni Mubarak amekaa madarakani tangu mwaka 1981-2011 alipopinduliwa, Ben Ali alikaa madarakani tangu mwaka 1987-2011 alipopinduliwa, Laurent Gagbo alikaa Madarakani tangu 2000-2011 alipopinduliwa. Charles Taylor hivyo hivyo, Yahya Jammeh miaka 22 alikuwa madarakani mpaka alipoondokewa kinguvu mwaka jana.

Orodha ni ndefu, lakini yote haya yanatokea wanayashuhudia huku bado baadhi ya viongozi niwakiwa na roho ngumu kweli kweli ya kung’ang’ania madaraka.

Togo kuna vuguvugu la kumtaka Rais Faure Gnassingbe aondoke madarakani kwani ameshindwa kuiendeleza nchi hiyo tangu arithi toka kwa baba yake alipofariki mwaka 2005.

Robert Mugabe ambaye iliaminika atafia madarakani ameng’oka, wengi hawaamini hasa wananchi wa Zimbabwe ambao mpaka muda huu bado wapo mitaani kusherekea anguko la Mugabe ambaye yupo madarakani tangu April 30, 1980.

Urais kwa Afrika unaonekana ni kazi rahisi, kwasababu kama ni kazi ngumu kwanini viongozi wengi wakiingia madarakani hawataki kuondoka? Rais wa 11 wa Marekani James Fox Knox aliwahi kusema “Presidency is not a bed of rosess” kwa tafsiri isiyo rasmi akimaanisha urais ni nafasi ngumu lakini kwa watawala wa Afrika wao wanapokuwa madarakani huwa hawawazi matatizo ya wananchi ila huwaza jinsi watakavyojineemesha wao na familia zao.

Rais unakaa madarakani miaka 30! Mugabe amekaa miaka 37 kuna lipi la maana alilolifanya? Napongeza Kagame ambaye ameshaweka wazi kuwa hatagombea 2024.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles