25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KHERI: SINA CHA KUJIFUNZA KWA SADIFA


Na EVANS MAGEGE -

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekamilisha harakati zake za kupanga safu ya uongozi wa juu huku jina la Kheri James liking’ara katika ngazi ya uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Kheri amerithi nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Sadifa Juma Khamis kwa miaka mitano.

MTANZANIA Jumapili limezungumza na kiongozi huyo na kuelezea mambo kadha wa kadha likiwamo suala la rushwa na mikakati yake ya kuuongoza umoja huo.

MTANZANIA Jumapili: Jina lako si maarufu sana katika medani za siasa za UVCCM, lakini liliibuka wakati wa mchakato wa uchaguzi, nini siri ya umaarufu huo wa ghafla?

Kheri: Ninachoweza kusema ni kwamba, siri kubwa ya umaarufu huo unaousema wewe ni umoja na mshikamano kwa vijana wenzangu ndani ya chama.

Siasa ndani ya chama nimezianza kuanzia ngazi ya tawi, kata hadi wilaya. Mapito yangu yote yalikuwa ya weledi wa hali ya juu kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi mbalimbali wa kisiasa katika ngazi nilizokutajia.

Nafikiri hatua hizo nilizopita zilirahisisha jina langu kufahamika vyema baada ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hiki.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini umeshinda wewe na si mwingine?

Kheri: Mungu ndiye alipenda nipate nafasi hii. Tulikuwa wagombea saba na wote walipata kura, ninaweza kusema wote tulishinda ila Mungu akanipa nafasi zaidi ya wenzangu.

Kumbuka mchakato wetu ulikuwa na watu zaidi ya 100, vikao vya chama vikachuja na kubaki saba hatimaye mimi  ndiye nikapata nafasi ya kuongoza umoja wetu wa vijana ndani ya chama.

MTANZANIA Jumapili: Kwa kawaida  mchakato wa uchaguzi mambo kadhaa hujitokeza yenye kuvunja au kutia moyo, vipi kwa upande wako uchaguzi ulikuwaje?

Kheri: Uchaguzi ulikuwa mgumu sana kwa sababu safari ilikuwa ndefu kufikia mafanikio. Ndani ya safari ya kupata mafanikio kulikuwa na ushindani wa hali ya juu sana kutokana na vijana tuliojitokeza kuwania nafasi hii,  tulikuwa wengi kila mmoja alikuwa na sifa zake. Haikuwa kazi rahisi kufikia ushindi huu. Kama nilivyoeleza awali Mungu ndiye aliyenifikisha hapa.

MTANZANIA Jumapili: Siku za nyuma uchaguzi wa UVCCM ulitawaliwa na makundi miongoni mwa vijana wenyewe na baadhi ya makada wakongwe, ambao iliaminika kuwa walikuwa na masilahi binafsi, vipi uchaguzi wenu hali ilikuwaje?

Kheri: Sina uhakika kama kulikuwa na hali hiyo kwa sababu sikuyaona mazingira hayo ndani ya mchakato, sijui labda kwa wagombea wenzangu kama waliona, kumbuka tulikuwa wagombea wengi sana.

MTANZANIA Jumapili: Inadaiwa kuwa mara nyingi vitendo vya rushwa hujitokeza wakati wa chaguzi zenu na mfano tumeshuhudia mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Sadifa Juma Hamis, amekumbwa na kadhia ya tuhuma za rushwa, unazungumziaje suala la rushwa?

Kheri: Sijui kwanini watu wanapenda rushwa wakati wanajua ni hatari kwa sababu inaminya haki za watu.

Kwa hili la rushwa kwenye chaguzi zetu napenda kuwaasa vijana wenzangu waache maisha ya kujirahisisha kwa kutegemea rushwa kutimiza malengo yao.

Rushwa ni saratani na Serikali ya Awamu ya Tano inapambana nayo usiku na mchana, kama kiongozi nawaasa vijana wenzangu kutambua kwamba Serikali ipo imara kupambana  na rushwa hivyo hawatakuwa salama kama wataendelea kuyaishi maisha ya rushwa kwa sababu hawajui siku wala saa ya kujikuta mikononi mwa Takukuru.

Nieleze wazi kuwa kitendo cha kushiriki kwenye vitendo hivi ni kujijenga katika misingi ya uadui wa maendeleo ya Taifa letu na mtu wa aina hiyo hafai katika jamii.

Vijana wenzangu wanatakiwa kutambua kuwa rushwa inaleta matabaka kwa sababu wengi haki zao zinakandamizwa kwa sababu ya fedha za kuhonga. Kwa UVCCM ninayokwenda kuiongoza nitakuwa mkali sana dhidi ya vitendo vya rushwa.

MTANZANIA Jumapili: Umejifunza nini kupitia kwa Sadifa baada ya  kukumbwa na tuhuma za rushwa siku moja tu kabla ya kufika tamati ya muda wake madarakani?

Kheri: Kwa msingi wa ulichokiuliza napenda kusema kwamba siwezi kujifunza chochote kwa Sadifa.

Unajuwa kila kitu unachokipata kinatokana na malengo uliyojipangia, binafsi nimejipangia kuongoza vijana wenzangu kwa weledi na masilahi mapana ya chama chetu. Hicho ndicho ninachoweza kusema kwa ufupi.

MTANZANIA Jumapili: Ukipewa nafasi ya kumzungumzia mwenyekiti aliyekutangulia, unaweza kumwelezea kuwa ni mtu wa namna gani?

Kheri: Siwezi kumwelezea yeye, labda ninaweza kujielezea mimi juu ya malengo ya uongozi wangu ndani ya UVCCM. 

MTANZANIA Jumapili: Malengo yako ni yapi?

Kheri: Yapo malengo matano ambayo kimsingi nikiyakamilisha naamini jumuiya yetu itakuwa bora zaidi.

Mosi; ni kuimarisha taasisi kisiasa kwa kuifanya iwe taasisi inayotumainiwa na vijana. Pili; kuwa wakili wa matatizo ya vijana wote nchini. Tatu; kuimarisha jumuiya kiuchumi ili ijitegemee bila kutegemea ruzuku. Nne; kuwawezesha vijana wote wenye uwezo wa kuwa viongozi kutimiza ndoto zao. Tano; kuisimamia Serikali katika mambo yote yenye masilahi kwa vijana. 

MTANZANIA Jumapili: Bavicha ni jukwaa jingine la vijana kutoka siasa za upinzani, umejipanga vipi kukabiliana nalo kisiasa?

Kheri: Si Bavicha tu hata vijana wa ACT-Wazalendo, CUF na NCCR-Mageuzi, wote sihitaji kukabiliana nao ila nahitaji ushirikiano nao kwa hoja zenye tija kwa nchi na maendeleo ya vijana.

Sisi ni ndugu lazima tuwe na malengo yenye tija kwa mustakabali wa vijana wa Taifa letu. Uongozi wangu utakuwa wa kipekee, nitatoa nafasi kubwa ya kushirikiana na upinzani lakini kama wakitaka kushindana najua wanajua CCM ina nguvu kubwa ya vijana hivyo tukipambana nao hawatatushinda.

MTANZANIA Jumapili: Ndani ya awamu hii ya tano, siasa za upinzani zinaonekana kupoa kama si kufifia kabisa hali ambayo ni tofauti na siku za nyuma, kwa mtazamo wako tatizo liko wapi?

Kheri: Kupoa kisiasa si tatizo ni jambo la wakati. Nasema hivyo kwa sababu kuu moja kwamba ajenda zilizokuwa zinatumika kuamsha hamasa,  zote zimefanyiwa kazi na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi na Serikali.

Kwa mtazamo wa jumla katika hoja hii ni kwamba wapinzani wameishiwa ajenda dhidi ya Serikali ya CCM, hivyo hawana budi kuja na ajenda nyingine zitakazo wapambanua tena kisiasa na kurejesha mvuto wa siasa zao kwa wananchi.

Leo hii Watanzania wanatambua vizuri jinsi Serikali inavyoshughulikia kero zao, sasa ukiibuka kuipinga CCM na Serikali yake wananchi wanakuona kama unapishana na gari la mshahara, watakuacha jinsi ulivyo nao wataendelea na safari ya kuiunga mkono Serikali kwa sababu inatimiza kile kilichokuwa kinawasumbua.

MTANZANIA Jumapili: Mali za UVCCM baadhi zinadaiwa kuyeyuka pia nyingine zipo, lakini mapato yake hayajulikani yanakokwenda, unadhani hali hiyo imetokana na nini?

Kheria: Rushwa, weledi hafifu wa uongozi umechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hili. Watu wamekuwa na tamaa na ubinafsi wa kujinufaisha na mali za jumuiya badala ya kuiongoza jumuiya.

Uongozi wangu umetoa mwezi mmoja wa kuchunguza na kutathmini mali zote za UVCCM baada ya kazi hiyo tutakuja na taarifa kamili ya nini kifanywe. Hivyo naamini kabisa baada ya mwezi mmoja tutakuwa na jibu sahihi la mali za jumuiya yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles