30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ALICHOKISEMA DK. MOLLEL SASA VS MWAKA MMOJA ULIOPITA

MAKALA haya ni mwendelezo wa makala ya wiki iliyopita. Desemba 15, mwaka huu, aliyekuwa Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel, alitangaza kukihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kurudi CCM.

Kimsingi makala haya yanazungumzia kauli ya Dk. Mollel aliyopata kutoa wakati akiwa Chadema mwaka mmoja uliopita na kauli yake ya sasa wakati amerejea CCM.

Akitangaza kujiuzulu ubunge wiki iliyopita, Dk. Mollel alisema uamuzi wa kujivua uanachama Chadema ni uamuzi wake mwenyewe, huku akiwa na akili timamu.

“Wakati naingia kwenye harakati za kugombea ubunge, niliamini kwamba pamoja na kupigania Wilaya ya Siha kupata maendeleo, lakini nitatumia fursa hiyo kulinda rasilimali za taifa letu.

“Dhamira yangu imeshindwa kuukataa ukweli huu, kuwa hivi sasa uongozi wa nchi yetu chini ya CCM umedhihirisha wazi kupigania rasilimali za nchi.

“Nimeona mbali katika maamuzi haya, kikubwa ninachotegemea wana – CCM mnipokee ili tuweze kupambana kulinda nchi na rasilimali zake,” hii ni sehemu ya kauli ya  Dk. Mollel.

Katika toleo lililopita pamoja na mambo mengine, Dk. Mollel alizungumzia sababu zilizomtoa CCM na kuhamia Chadema.

Miongoni mwa sababu hizo ni hujuma alizofanyiwa na wana-CCM.

Pamoja na mapito mengi aliyoyaeleza Dk. Mollel ambaye alipata kuwa Mganga Mkuu katika Hospitali ya Manyara, alisema misukosuko ya kisiasa ilisababisha afukuzwe kazi.

Endelea kufuatilia mahojiano haya maalumu yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana kati ya mwandishi wa gazeti hili, RACHEL MRISHO na Dk. Mollel… 

MWANDISHI: Unazungumziaje hali ya kisiasa nchini?

Dk. Mollel: Tunapita katika kipindi kigumu sana kisiasa. Hali ya kisiasa nchini mwetu si shwari, ila Watanzania wasihofu, waombe Mungu maana Tanzania ipo kwenye hali inayofanana na uchungu wa uzazi. Unajua ili nchi iweze kuamka na kupata demokrasia ya kweli na haki, sisi Watanzania lazima tupite katika magumu ambayo tunayapitia. Kwa sasa Tanzania inaelekea katika kushinda, silaha yetu kubwa ni kushikamana kwa upendo ili kuishinda vita tuliyonayo ya kisiasa. 

MWANDISHI: Ni changamoto gani zipo katika Jimbo la Siha?

Dk. Mollel: Changamoto kubwa ni katika uwekezaji kwenye ardhi, nitapenda nizungumzie kwa upana suala hili.

Katika jimbo letu kuna ushirika unaitwa Siha Kiyeyo, kazi yake ilikuwa ni kukuza kilimo cha kahawa.

Ushirika huo hivi sasa umekuwa ni kikundi cha watu wanaonufaika wenyewe. Najaribu kushirikiana na wenzangu wa serikali kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa kwa manufaa ya wanaushirika wote na si kikundi kama ilivyo hivi sasa.

Kuna ubadhirifu mkubwa umebainika katika eneo hilo, hivi karibuni tumesikia mwenyekiti wa ushirika, DC ambaye hivi sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara anatakiwa arudishe fedha za ushirika. Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamemtaka afanye hivyo. Hata mkurugenzi aliyetoka Siha amepelekwa mahakamani anatakiwa arejeshe fedha za ushirika, kuna orodha kubwa ya ubadhirifu kwenye mashamba ya ushirika.

Mwaka 2014 walipanga kuuza shamba la Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa Mkoa Kilimanjaro (KNCU), linaloitwa Kiraragua, wakakubaliana kuliuza.

Ukweli sisi hatupingi uwekezaji, ila shamba hilo walishaliuza tangu mwaka 2014 walipoona mchakato wa kulipana unaingiliana na shughuli za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Hii ina maana gani, ni kwamba kuna harufu ya rushwa.

Shamba hilo lina maji mengi ambayo yanaweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji, ni shamba ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilimwa na mtu mmoja kwa kukodishiwa na KNCU, inasikitisha sana leo linakuja kuuzwa kwa ajili ya kulipa deni la CRDB.

Ikumbukwe kwamba, watu wa Siha walikuwa wanakodishiwa kila mwaka na kulipa Sh 50,000, najiuliza, hizi fedha ambazo zilikuwa zinalipwa, kwanini zilikuwa hazilipi hilo deni?

Tangu nikiwa mdogo nilidhani huyo aliyekuwa amekodishiwa ndiye mwenye shamba, kumbe ni shamba la ushirika. Hilo shamba kama lingekuwa linalimwa kahawa kwa muda wote huo wa miaka zaidi ya 30 Ushirika ungekuwa mbali sana kimaendeleo.

MWANDISHI:  Nini ushauri wako kwa Serikali? 

Dk. Mollel:  Kwanza deni la CRDB lihakikiwe upya kwa kushirikisha wadau. Awali wakati wa uhakiki walikaa kirafiki wamenitenga mimi kama mbunge, waziri alikwenda kimya kimya, hawajanishirikisha na wala sifahamu nini kimeamriwa.

Ila ninachofahamu maamuzi ya mwaka 2014 bado yanatekelezwa, nasikia kuna mambo yanaendelea ya kuliuza.

Wana- Siha hatuna chuki na wawekezaji, anayegombana na wawekezaji hataki maendeleo, tunachotaka kufahamu hilo shamba likiuzwa Wanasiha wanapata nini?

Maana anayeuziwa ni huyo huyo anayelalamikiwa katika ubadhirifu wa fedha uliofanyika kwenye ushirika wa Siha Kiyeyo.

 Tunachosema wanauza kwa minajili ipi, na bei inayouzwa ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa ardhi wenye ekari zaidi ya 3,824.

Inadaiwa kwamba, baada ya mauzo fedha hizo zitapelekwa kwenye akaunti maalumu ya Escrow, sisi tuna shaka kwa sababu fedha zikipelekwa Escrow huwa zinaibiwa, ni mbinu chafu. Nimemshauri ofisa mrajisi mkuu walinusuru shamba hilo, nikamwambia likiuzwa jambo litakalokuja ni kuigharimu serikali huko mbele.

Tunahoji kwanini Serikali isilichukue hilo shamba kwa KNCU na kulipa deni la CRDB na hilo shamba liendelezwe kwa manufaa ya wananchi wa Siha? Naishauri Serikali itengeneze mkakati maalumu wa kuanzisha benki ya ushirika kwa Wilaya ya Siha pamoja na kuanzisha benki ya ushirika Mkoa wa Kilimanjaro. Hiyo itawasaidia wananchi wengi badala ya kikundi cha watu wachache. 

MWANDISHI: Serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa madawati, vipi hali ikoje katika jimbo lako katika sekta nzima ya elimu?

Dk. Mollel:  Suala la madawati tumeshamaliza, hakuna rekodi ya mwanafunzi kukaa chini. Kwa upande wa shule za msingi kuna changamoto kubwa ya uchakavu wa majengo na shida ya ujenzi wa maabara.

Tunapambana kuhakikisha sekondari zote ziwe za bweni, hasa kwa ajili ya watoto wa kike, kwa sababu wanapokwenda shuleni na kurudi nyumbani wanakutana na vikwazo vingi.

Uzoefu unaonyesha watoto wanaokaa nje ya mabweni wana changamoto ya kupata ujauzito, kukosa muda wa kujisomea, kuolewa kabla ya muda, hata ufaulu wao huwa mbaya.

Kwa sasa ujenzi wa mabweni ndio mpango mkakati wangu. Tunatamani tuongeze shule za sekondari. Tumeshaanza kujenga mabweni katika shule ya Nuru na kuanzisha harambee kwa ajili ya kujenga mabweni. Zipo shule nyingi ambazo zina mpango unaofanana.

Tumeelekeza fedha za mfuko wa jimbo katika shule za msingi. Kuna shule ilikuwa ya mabanzi tumelazimika kujenga vyumba viwili vya madarasa pamoja na kufanya ukarabati katika baadhi ya shule za msingi zilizopo katika kata 17.

Katika utawala wangu nimetembelea kata zote na kufanya chagizo kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati kwa shule ya msingi na sekondari.

Nimepeleka mabati 100 katika Shule ya Sanya Hoye kwa ajili ya kuanzisha shule ya msingi, mtindo huo tumefanya katika kata zote 17, Sanya ndiyo imepata mgawo mkubwa kutokana na idadi kubwa ya watu, watoto ni wengi zaidi.

MWANDISHI: Maeneo mengi vijijini kuna migogoro ya wakulima na wafugaji, hali ikoje katika lako?

Dk. Mollel: Kimsingi Siha hakuna migogoro ya wakulima na wafugaji, bali kuna mivutano midogo midogo ya majirani.

Jimbo la Siha lina watu ambao wao wenyewe ni wakulima, pia ni wafugaji, katika mazingira hayo huwa wanaingiziana mifugo katika mashamba na anayeingiza huwa ni mkulima.

Kwa upande wa ardhi, kuna matatizo kadhaa. Mosi ni tembo kuharibu mazao, pia wawekezaji kuhodhi ardhi kubwa.

Kuna maeneo ya serikali kiongozi anachukua ekari 200 analima peke yake, tunahitaji kuwapo na utaratibu mzuri wa matumizi ya ardhi ili kila mwananchi apate eneo la kulima, hata kama ya kukodishwa, wanyonge ndio wapewe, tunataka kuishauri serikali ifanye hivyo.

Katika maeneo ya Serikali yaliyopo chini ya halmashauri na ya ushirika tunaona serikali ikodishie wananchi kwa uwiano sawa, ili wananchi waweze kujikimu.

Katika uchunguzi tulioufanya tumebaini kwamba baadhi ya viongozi wamelima ardhi kubwa bila kulipia halmashauri.

Hali hiyo tunataka tuiondoe, tunataka ardhi inufaishe wote na si wakubwa peke yao. Ni kosa mtu kulima eka 100 bure ilhali wapo wananchi wenye uwezo wa kulipia.

Kuna tatizo la kuwatisha wawekezaji Siha, wenzetu upande wa pili wanawatisha wawekezaji kisiasa, kwamba Chadema imeingia madarakani kwa ajili ya kuwanyang’anya watu ardhi.

Hatuwezi kumnyang’anya mtu ardhi anayemiliki kisheria, tunapinga uwekezaji usio na tija kwa wana-Siha, kama mwekezaji anawekeza bila maslahi kwa Wanasiha, hatuko tayari kuliona hilo.

Tunaishauri Serikali hasa wizara ya ardhi na kilimo kwamba ardhi ya Kilimanjaro ni ndogo sana lakini ina idadi kubwa ya watu, wanavyofikiria ardhi ya Kilimanjaro wasiichukulie kama ni ardhi ya mikoa mingine.

Pili, wachunguze kila jambo wanaloelezwa, ardhi ya Kilimanjaro isipotumika vizuri inaweza kusababisha maafa baadaye, ardhi ina akiba kubwa ya maji kwa ajili ya Siha na Hai, pia kwa ajili ya Bonde la Pangani.

Uwekezaji unaowekezwa ndani ya Siha una historia ya kukausha mito, wajue kwamba hatukatai maendeleo ya uwekezaji, tunakataa uwekezaji wa kifisadi, ambao hauna tija kwa taifa, na wananchi kutofaidi bali ni wawekezaji wajanja.

MWANDISHI: Kuna dhana kwamba maeneo yanayoongozwa na upinzani miradi mingi hukwama, vipi hali hiyo katika Jimbo la Siha.

Dk. Mollel: Niseme tu miradi inaendelea vizuri, kuna miradi mikubwa ya barabara inakuja, wananchi wasubiri na baadhi ipo katika hatua ya utekelezaji.

Hadi sasa hakuna mradi uliokwama, miradi mingi tumeshaianzisha, wananchi wawe na subira, mpaka sasa kuna mradi mkubwa unaanza mwezi huu na kuna barabara zaidi ya 20 zinajengwa na makatapila yapo tangu Desemba, mwaka jana.

Barabara zimeanza kujengwa katika kata tofauti na kuna mradi mkubwa wa daraja wa kuunganisha Kata ya Ivaeli na Kashashi, Daraja la Kisube, ujenzi wake utagharimu Sh milioni 960.

MWANDISHI: Kumekuwapo na malalamiko mengi katika sekta ya afya, hasa ukosefu wa dawa na majengo, je; hali ikoje katika eneo hilo

Dk. Mollel: Ni kweli sekta ya afya ina changamoto nyingi, nilipoingia madarakani kama mbunge nimekuta hospitali ilijengwa jengo la wagonjwa wa nje, maabara na jengo la utawala, haina jengo la kulaza wagonjwa na haikuwa na fungu la dawa kwa maana ya kutoka Bohari Kuu ya Dawa – MSD.

Serikali Kuu, kwa kushirikiana na viongozi wenzangu wa wilaya, tulifuatilia pamoja na juhudi za mganga mkuu tulishirikiana, hivyo mwaka huu fungu la dawa limeanza kutolewa, awali tulikuwa tunatumia fungu la dawa kutoka Hospitali ya Kibong’oto, ile ni hospitali ya taifa.

Tunapanga kupata wodi ya kulaza wagonjwa na kupata chumba cha upasuaji, wodi ya kina mama na watoto, tunapambana ili iweze kupatikana.

Tumepanga katika kanda sita katikati ya kila kata mbili kuwe na kituo cha afya, lakini kila kata kuwe na zahanati yake.

MWANDISHI: Wana-Siha watarajie nini kipya kutoka kwako ili wawe na matumaini juu yako.

Dk. Mollel: Wapigakura wangu watarajie uongozi shirikishi katika kutoa maamuzi ndani ya wilaya yao na si watu wachache kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Pia watarajie kwamba, hatutakuwa watu wa matabaka kupitia itikadi za kisiasa, ipo dhana iliyojengeka kuwa ukiwa tofauti na chama unachokiongoza unakuwa mwananchi wa daraja la pili.

Katika utawala wangu, uwe CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo au CUF, unakuwa mwananchi wa Siha. Si vinginevyo.

Haya mambo ya kugawa watu kupitia vyama nitapinga kwa nguvu zote na niombe washirikiane nami kukataa kugawanywa kwa itikadi ya vyama.

Katika suala la maendeleo, sipendi kusema sana, bali watumie muda wao kuona na si kunisikiliza kimefanyika nini.

Wataona makubwa sana, kwani naamini tulianza na Mungu na tutafanya na Mungu, wapo wenzetu wamejipanga wakiamini kwa kutumia nguvu ya vyama vyao na nguvu zao wanaweza kukwamisha maendeleo ya Siha.

Wanapita huku na kule wakidai kuwa hakuna maendeleo yatakayofanyika, wawapuuze.

Nawaonya wasije wakatafuta mkono wa Mungu, wanapopambana na mimi wasifikiri wananikomoa mimi, wajue utawashukia mkono mzito wa Mungu.

Mimi nitasimama imara na watajuta wakianzisha hiyo kampeni. Mimi ni mbunge wa wana-Siha wote na Rais Magufuli si wa CCM.

Naomba tuungane pamoja kuleta maendeleo kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles