BANJUI, GAMBIA
SERIKALI ya Gambia imetangaza kuanza kufanya uchunguzi wa maovu yaliyofanywa wakati wa utawala wa kiongozi wa zamani wa kidikteta, Yahya Jammeh.
Jopo la tume inayojulikana kama Tume ya Ukweli, Upatanisho na Marekebisho (TRRC), linakabiliwa na matarajio makubwa ya kuleta haki katika taifa hilo dogo linalopambana kuleta maendeleo ya kidemokrasia.
Lakini hadi sasa bado haikuwekwa wazi kama kweli Jammeh ambaye yupo katikati ya uchunguzi huo atasimamishwa mbele ya mahakama.
Kwa miaka 22 ya uongozi wa Jammeh, taifa hilo lilishuhudia ukandamizaji uliogusa karibu kila sehemu ya jamii ikiwa ni pamoja na mauaji, kutoweka kwa watu, unyanyasaji wa kijinsia, mateso pamoja na watu kuwekwa vizuizini.
Hali hiyo ilikomeshwa pale Jammeh alipolazimika kuondoka madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2017 na kiongozi wa upinzani, Adama Barrow.