32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rais wa Burundi mafichoni

rais nkurunzinzaWaaandishi Wetu, Bujumbura na Dar

WAKATI makundi hasimu ya askari nchini Burundi yakipambana vikali kugombea kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bunjumbura, Rais Pierre Nkurunzinza yuko mafichoni kusikojulikana.

Hayo yamefahamika huku kukiwa na utata na mkanganyiko mkubwa kuhusu mafanikio ya jaribio la mapinduzi lililoongozwa na Meja Jenerali Godefroid Niyombare.
Jenerali Niyombare ambaye pia ni balozi wa zamani wa Burundi nchini Kenya alitimuliwa ukuu wa usalama na Nkrunzinza Februari mwaka huu ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Mapambano makali zaidi katika kuwania udhibiti wa mji mkuu wa taifa hilo yalionekana zaidi katika jengo la Kituo cha Taifa cha Redio Burundi (RTNB), ambako matangazo yalikatishwa kwa muda.

Taarifa zilisema kuwa kituo hicho cha habari kilikuwa chini ya udhibiti wa vikosi vinavyomtii Rais Pierre Nkurunziza, huku wanajeshi watano wakiripotiwa kuuawa katika mapambano hayo.
Mkuu wa Majeshi, Prime Niyongabo ambaye ni mtiifu kwa Rais Pierre Nkurunziza aliviambia vyombo vya habari kuwa askari wake walikuwa wanadhibiti maeneo muhimu ukiwamo uwanja wa ndege, lakini viongozi wa mapinduzi walisisitiza wao ndiyo walikuwa wanadhibiti maeneo hayo.
Machafuko hayo yalianza baada ya Nkurunziza kutangaza kugombea urais kwa muhula wa tatu kinyume na Katiba na makubaliano ya amani ya Arusha.

Uamuzi wake huo ulisababisha wiki kadhaa za maandamano yaliyoshuhudia watu 20 wakiuawa.

Nkurunziza aibuka

Ingawa Rais Nkurunzinza aliweza kuibuka jana mchana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu jaribio la kumpindua akilaani vikali kitendo hicho kupitia RTNB, mahali alipo bado pamebakia kuwa siri.

Wakati akizungumza kwa njia ya simu na RTNB kabla ya matangazo ya redio hiyo ya taifa kukatishwa, Nkurunzinza alisema bado analiongoza taifa hilo na yuko tayari kusamehe askari watakaoamua kujisalimisha.

“Nalaani vikali kundi la wala njama za mapinduzi,” alisema Rais Nkurunziza, ambaye alikuwa Tanzania wakati jaribio la mapinduzi lilipotangazwa juzi.

“Nawashukuru askari ambao wanaweka hali katika utulivu na namsamehe askari yeyote atakayeamua kujisalimisha,” Nkurunzinza alisema akiwa mafichoni.

Awali kiongozi huyo wa zamani wa waasi wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyomalizika mwaka 2005, aliondoka katika mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) jijini Dar es Salaam ili kurudi nyumbani baada ya taarifa ya kupinduliwa juzi.

Azuiwa kuingia Burundi

Hata hivyo, ndege yake ilizuiwa kuingia katika anga ya Burundi juzi jioni, kwa vile uwanja wa ndege wa Bujumbura ulifungwa kwa amri ya Jenerali Niyombare.

Inasemekana ndege yake ilitua kwa muda mjini Entebbe, Uganda kabla ya kugeuza kurudi Tanzania ambako awali inadaiwa alikaa katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, kabla ya kuhamishwa mahali kusikojulikana.

Vyanzo viwili vya habari nchini, vilithibitisha kuwa Nkurunzinza yuko Dar es Salaam. Kimoja kilisema yuko katika ‘eneo salama’ lakini bila kulitaja.

Matangazo yakatwa

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa RTNB, Jerome Nzokirantevye, matangazo wakati Nkurunzinza akizungumza, yalikatishwa kutokana shambulio kali kutoka kwa askari wanaounga mkono mapinduzi.
“Tulishambuliwa. Ni shambulio kali. Mtambo wa kurusha matangazo ulikatwa. Hatuwezi kurusha matangazo,” mkurugenzi huyo alisema.

Lakini baadaye matangazo yalirudi, huku yakianza kwa kupiga muziki kabla ya kutoa taarifa kuwa askari watiifu kwa Rais Nkrunzinza walikuwa bado wanakidhibiti.

“Tulisimamisha matangazo wakati wa shambulio. Sasa mapigano yamesimama na tunaweza kuanza matangazo. Ni askari watiifu wanaokidhibiti pamoja na maeneo mengine nyeti,” Nzokirantevye alisema, taarifa ambayo ilithibitishwa na mashuhuda mjini Bunjumbura.

Harakati za kutafuta udhibiti wa kituo hicho ulikuja baada ya usiku wa kuamkia jana wale wanaomtii Nkurunziza kuharibu vituo kadhaa binafsi ambavyo vilitumiwa na waasi kutangaza ujumbe wao.

Redio yalipuliwa

Miongoni mwa vituo hivyo binafsi ni Burundi Isanganiro, ambacho kiliteketezwa kwa moto.

Kwa mujibu wa Jenerali mmoja anayeunga mkono jaribio hilo la mapinduzi, vitengo vinavyopigana kumpindua Rais Nkurunzinza vilipata agizo la kuiteka RTNB kwa namna yoyote.
Kuna madai kuwa kundi la vijana linalounga mkono serikali ndilo lililoshambulia vituo binafsi vya redio mjini Bujumbura.

Kundi hilo linalojulikana kama Imbonerakure, baadhi ya watu wanaamini linatumiwa kama wapiganaji na huenda limepewa silaha kuwatishia raia kabla ya uchaguzi.
Lakini chama tawala cha CNDD-FDD kimekana madai ya kuhusika na wanamgambo hao.

Licha ya hayo hali bado ni tete nchini Burundi siku moja baada ya Jenerali Godefroid Niyombare kujaribu kufanya mapinduzi.

Barabara nyingi zimeendelea kuwa bila wazi kwa kipindi kirefu huku watu wengi wakibaki majumbani mwao wakihofia usalama wao.

Mapambano ya risasi yalikuwa yakiendelea hadi gazeti hili linaenda mitamboni jana, huku milipuko kadhaa ikisikika.
Walioshuhudia mjini Bujumbura walisema walisikia mapigano makali baina ya askari watiifu kwa rais na wale wanaounga mkono mapinduzi.

“Hatukulala usiku kwa sababu ya hofu. Milio mingi ya mabomu na risasi inasikika kila mahali. Na watu wamejawa na hofu,”mmoja wa walioshuhudia aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyomalizika mwaka 2005, jeshi lililokuwa likidhibitiwa na Watutsi ambao ni wachache nchini humo, lilipambana na makundi ya waasi wa Kihutu walio wengi likiwamo CNDD-FDD lililoongozwa na Nkurunziza.

Baada ya hapo jeshi lilivunjwa na kuundwa upya kwa kuchanganya makundi hasimu, lakini kasoro katika ngazi mbalimbali za jeshi hilo bado zinaonekana.

Hata hivyo, tofauti zilizopo katika jeshi la Burundi kufuatia jaribio hilo la mapinduzi hazionekani kuwa katika misingi ya ukabila.

Mkuu wa Majeshi Prime Niyongabo aliye mtiifu kwa Nkurunzinza pamoja na Jenerali Niyombare aliyetangaza mapinduzi wanatoka kabila moja la Kihutu.

Makundi hayo yanaonekana kugawanyika kati ya wale wanaoamini Nkurunziza alikiuka makubaliano ya amani kwa kutaka kuongoza kwa muhula wa tatu na wale wanaobakia kuwa watiifu kwake.

UN yaingilia kati

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki Moon ametoa wito wa dharura kwa pande zote nchini Burundi kuonyesha utulivu na kujizuia kufuatia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Nkurunzinza.
Msemaji wake, Stephanie Dujarric amesema Ban amesisitiza haja kwa viongozi wote wa Burundi kudumisha amani na usalama katika taifa ambalo limekumbwa na matukio ya ghasia mbaya katika kipindi kilichopita.

Serikali ya Marekani
Serikali ya Marekani imewataka Warundi kuweka silaha chini huku Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani, Josh Ernest akisema nchi yake inafuatilia matukio nchini Burundi kwa makini na wasiwasi.

Alisema Marekani bado inamtambua Nkurunzinza kuwa kiongozi rasmi wa Burundi lakini inamtaka aheshimu katiba ya taifa hilo na mikataba ya amani ilyofikiwa mwaka 2005 kwa kutogombea muhula wa tatu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na lile la Amani la Umoja wa Afrika kila moja kwa wakati wake yalikuwa yakikutana jana kujadili mgogoro huo wa Burundi.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliokutana Dar es Salam juzi tayari wamelaani jaribio hilo la kutaka kumuondoa madarakani Rais Nkurunzinza na kutaka arudishwa kwa mujibu wa sheria.

Kauli ya CNDD-FDD
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu kutoka Bujumbura, Msemaji wa Chama tawala cha CNDD-FDD, Ndabirabe Gelose, alisema pamoja na kufanyika jaribio la mapinduzi ya Serikali ya Rais Nkurunziza, chama hicho hakitabadili mgombea wake.

Alisema makundi yanayochochea uasi dhidi ya Serikali ya Nkurunziza lengo lao ni kutaka kuundwa Serikali ya mpito jambo ambalo wao hawaliungi mkono.
“Ninachotaka kukwambia ni kwamba msimamo wa CNDD-FDD ni uko pale pale, hatubadili mgombea wetu urais … sisi bado tunamtambua Nkurunziza.

“Na tunalishukuru jeshi kuingilia kati ili kurejesha hali ya amani nchini kwetu ingawa bado hatuwezi kusema hali imetulia moja kwa moja kwa sasa,” alisema Gelose.

MTANZANIA ilipomuuliza alipo Rais Nkurunziza, msemaji huyo wa chama tawala alishindwa kueleza mahali alipo kiongozi huyo.

“Siwezi kusema alipo Rais Nkurunziza na hili ni kwa ajili ya usalama ndugu yangu. Tunajua hawa wanaleta vurugu lengo lao haliwezi kufanikiwa, sasa wameamua kukamata baadhi ya redio kusema mambo yao,” alisema.
Membe azungumza
Rais Nkurunziza ameendelea kujificha mafichoni akihofiwa kubainika na wabaya wake.

Akizungumza waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alisema hawezi kuzungumzia mahali aliko Rais huyo kwa sasa kwa kuhofia kujulikana na mahasimu wake.

“Unajua kwa sasa anawindwa na wabaya wake hivyo itakuwa vigumu kutolewa taarifa za mahali ambako amekimbilia rais huyo,”alisema.

Membe alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na taarifa zilizozagaa kwamba Rais Nkurunziza yuko nchini kwa lengo la kutafuta hifadhi.

Akizungumzia hali ya Burundi ilivyo sasa baada ya kutangazwa mapinduzi, Waziri Membe alisema hadi sasa hali bado tete nchini humo.

Membe alisema hali tete ya suala hilo ilisababisha viongozi wakutane juzi kutafuta ufumbuzi wa kudumu na kurejesha amani.

“Sisi Tanzania tunawaomba wananchi wa Burundi watulie na kuchagua viongozi wa nchi yao kwa njia ya amani kama nchi nyingine zinavyofanya,” alisema.
Alisema Rais Jakaya Kikwete, katika mkutano wa juzi na baadhi ya viongozi wa Afrika Mashariki aliwaeleza kwamba bara hili halitakuwa tayari kuona nchi yoyote inapata kiongozi kwa njia ya mapinduzi.

Alisema Baraza la Mawaziri waliokutana juzi litakutana tena Jumatatu ijayo na litatoa taarifa ya hali ilivyo nchini Burundi.

“Kuanzia sasa sitazungumzia hayo hadi baraza letu litakapokutana hiyo Jumatatu,” alisema.

Wabunge na mgogoro Burundi
Wabunge wa Bunge la Tanzania wametofautiana kuhusu mgogoro wa siasa nchini Burundi ambako baadhi yao wameunga mkono hatua ya jeshi la nchi hiyo kupindua Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza na wengine wamepinga hatua hiyo
.
Wakizungumza na MTANZANIA jana katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma, wabunge wengi walionekana kutofurahishwa na kitendo hicho, huku wakitoa wito kwa viongozi wa Afrika kujenga utamaduni wa kuheshimu Katiba za nchi zao.

Kwa mujibu wa wabunge hao, machafuko ya siasa nchini Burundi yametibua sifa kubwa aliyojijengea rais huyo miaka 10 iliyopita, hali iliyosababisha kupewa tuzo kutokana na kusaka amani nchini humo.

Mbunge wa Manyoni Magharibi, Paul Lwanji (CCM), alisema kilichotokea Burundi ni kielelezo cha viongozi kuamini katika nguvu zaidi, badala ya kuzingatia dhana ya maridhiano.

Hata hivyo, Lwanji alisema Tanzania haina jambo la kujifunza kutoka Burundi isipokuwa Burundi ina jambo la kujifunza kutoka Tanzania.

“Mapinduzi ya Burundi sura yake haijajulikana vizuri, kuna mambo mengi pale; masuala ya ukabila, madaraka na mengine lakini nasema utaratibu wa kuheshimu Katiba ni mzuri.
“Tanzania tumekuwa na utaratibu marais wetu wakimaliza muda wao wanaondoka, awamu ya nne anamaliza muda wake na sasa tunajiandaa kuchagua awamu ya tano ndiyo maana nasema Burundi inapaswa kujifunza kutoka Tanzania si Tanzania ijifunze kutoka Burundi,” alisema.

Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo (CCM), alisema: “Rais Nkurunziza amefanya kosa na jeshi nalo limefanya kosa kufanya mapinduzi…kosa moja halihalilishi kosa jingine.
“Tayari yalikuwapo mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro, jeshi walipaswa kusubiri matokeo ya mazungumzo ya wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.
“Nkurunziza alipata tuzo kutokana na jitihada zake za kujenga amani nchini Burundi lakini kwa machafuko haya sifa zile zimeporomoka. Kazi aliyoijenga kwa miaka 10 ameivuruga mwenyewe,” alisema.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alisema kilichofanyika Burundi ni dhambi ya kutokuheshimu Katiba na si jambo jingine.

“Mapinduzi si kitu kizuri, lakini kudharau Katiba ni kitu kibaya sana, sasa kama jeshi limepindua nchi ili kusimamia Katiba kulingana na matakwa ya wananchi, basi jeshi hapa is a good devil (shetani mzuri),” alisema.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema hakuona sababu za wananchi wa Burundi kuandamana na kufanya vurugu mitaani kupinga Rais Nkurunziza asigombee muhula wa tatu.

“Mahakama imesema Nkurunziza anayo nafasi nyingine ya kugombea kwani muhula huu ni wa pili si wa tatu kama inavyodaiwa, hapa hakuhitajiki nguvu kubwa kuelewa.

Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), alisema mgogoro huo wa siasa ni funzo kwa viongozi wa Afrika, huku akiwataka Warundi kuiga mfano wa Tanzania.
“Tanzania imepigania amani ya Burundi kwa muda mrefu tangu enzi za Mwalimu Nyerere ni vema wenzetu wakaiga mfano wa Tanzania… jingine ni kuheshimu Katiba na hili ni kwa nchi zote za Afrika,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Joseph Hiza, Shaban Matutu (Dar) na Khamis Mkotya, Dodoma

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles