25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa: Ninachunga ulimi wangu

benjamin mkapaNA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa, amesema kwamba yeye ni mwanasiasa mstaafu anayechunga ulimi wake.
Mkapa alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipofungua mkutano wa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).
Alisema pamoja na hali hiyo hivi sasa kila anapopelekewa mialiko ukiwamo wa CRB huwa anajiuliza kukubali lakini hujikutuka akipata moyo kwa kuchunga ulimi wake.
“Nilipoombwa kuja kuwa mgeni rasmi katika mkutano huu nilisita sana kukubali mwaliko wenu lakini nilitiwa moyo nilipokumbuka tukio moja.
“Mtoto mmoja aliwahi kumuuliza baba yake, je, nani ni bingwa wa kuongoza shughuli za Serikali, alijibiwa kuwa ni mwanasiasa mstaafu aliyehitimu na kuchunga ulimi wake…hapo nikapata ujasiri wa kuitikia ombi lenu,” alisema Mkapa na kushangiliwa na makandarasi.
Akizungumzia suala la mikataba ya uchumi, Rais Mkapa, alisema anaipinga hasa ile inayohusu Tanzania na nchi za Ulaya kwa sababu huwanyima Watanzania haki ya kujiendeleza badala yake nchi hizo ndiyo hujiendeleza zenyewe.
“Wao wanaweza kuja hapa na wakashinda zabuni mbalimbali. Je, wewe ukienda Ulaya utashinda? Wanasema kutakuwa na usawa sasa hapo ni usawa gani huo, napinga kabisa kwa sababu ni njia ya kuhakikisha…hahaha mmenielewa,” alisema.
Mkapa alishauri Serikali kuwapa upendeleo maalumu wakandarasi wa ndani itakapoanza kulipa malimbikizo ya madeni wanayoidai.
Alisema hata kazi kubwa na nyingi za ujenzi wanapaswa kupewa wazalendo kwa kuwa kuna faida nyingi na fedha zinabaki nchini na kuleta maendeleo endelevu.
“Wakandarasi wazalendo wawezeshwe na wakamate soko la ujenzi kwa sababu wana uwezo ndiyo maana naona katika malipo ya malimbilizo ya madeni naomba Serikali iwape upendeleo maalumu,” alisema Mkapa.
Akizungumzia kitabu alichokiandika alisema: “Uhandisi niliofanya ni kuchapisha hotuba zangu zote za miaka 10 ya uongozi wangu lakini sikiuzi na wala sitaki kukinadi”.
Katika mkutano huo bodi hiyo ilimkabidhi Mkapa zawadi ikiwamo kalamu ambako alisema: “Nashukuru kwa zawadi mliyonipa pamoja na kalamu, matokeo yake mtayaona kwa sababu nguvu ya akili bado ninayo”.
Naye Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema Rais Jakaya Kikwete ameahidi kulipa madeni yote ya wakandarasi kabla ya kumaliza muda wake.
Alisema anatambua madai yote ya wakandarasi hivyo imeweka mipango katika bajeti ya mwaka huu kuhakikisha yanalipwa yote.
“Hakuna Serikali yoyote isiyodaiwa duniani, hakuna tajiri asiyedaiwa na Serikali ya Kikwete ni tajiri ndiyo maana inadaiwa,” alisema Dk. Magufuli.
Awali, Mwenyekiti wa CRB, Consolata Ngimbwa, alisema tatizo la wakandarasi kutolipwa mapema limesababisha baadhi yao kufunga ofisi kwa kuwa wamefilisika.
Alisema ni vema Serikali ikawa inatangaza zabuni za ujenzi kukiwa na uhakika wa fedha kwa sababu wakandarasi wengi wamekuwa wakikwama kutokana na kutolipwa kwa wakati.
Msajili wa ERB, Steven Mlote, alisema viapo walivyoapa wahandisi vinawalinda wasikiuke maadili ya kazi zao.
Alisema wahandisi wanaoonekana kutokuwa na maadili na kwenda kinyume na matakwa ya taaluma zao wamekuwa wakifutiwa usajili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles