24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Uhuru akwepa kuzungumzia ufisadi wa nduguze

uhurukenyattaNAIROBI, KENYA

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ameendelea kukwepa kuzungumzia kashfa ya ufisadi wa Sh bilioni 5.1 katika Wizara ya Afya, ambako baadhi ya jamaa zake wametajwa kuhusika.

Ikiwa ni siku nne tangu kuibuliwa kwa sakata hilo, katika taarifa yake ya kila wiki kwa wanahabari, Msemaji wa Ikulu, Manoah Esipisu, aliepuka kuitaja kashfa hiyo inayoendelea kuchunguzwa na Tume Huru ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na kuzua hisia kali kwa umma.

Esipisu aliyetoa taarifa hiyo akiwa Khartoum, Sudan alikoandamana na Rais Kenyatta kwa ziara rasmi, aliangazia zaidi ziara hiyo ya Sudan na ile iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na Wakenya ya Rais wa Tanzania, John Magufuli iliyoanza jana.

Akizungumzia kashfa hiyo ya ufisadi juzi Jumapili, Waziri wa Afya Dk. Cleopa Mailu, alisema hakuna fedha zilizopotea katika wizara hiyo akisema ripoti ya uhasibu iliyoangaziwa na vyombo vya habari ilikuwa ya kupotosha.

“Wizara ingependa kufafanua kuwa madai ya ripoti ya uhasibu hayakuwa na kweli na yalifasiriwa visivyo,” alisema Dk. Mailu akihutubia wanahabari jijini Nairobi akiwa ameandamana na katibu wa wizara hiyo Dk. Nicholas Muraguri.

Alisema sheria ilifuatwa katika kutoa zabuni na kutoa malipo kwa kampuni zilizotajwa katika ripoti hiyo kwa kupokea mamilioni ya fedha kwa njia ya kutiliwa shaka.

“Tulihusisha Bunge na Wizara ya Fedha kwa mujibu wa sheria na kwa hivyo kufikia sasa habari zilizosambazwa kwa umma si za kweli,” alisema.

Dk. Mailu alisema japo hakufurahia jinsi ripoti ya uhasibu ilivyofikia wanahabari bila masuala yaliyotiliwa shaka kufafanuliwa, atawaalika wahasibu huru kufanya uchunguzi.

“Ikitokea kuna mtu aliyehusika kwa njia yoyote na matumizi mabaya ya fedha kwa njia ya ulaghai au wizi, basi sheria itachukua mkondo wake. Hata hivyo, kufikia sasa hakuna pesa zilizopotea,” anasema

Alipoulizwa kwa nini zabuni na malipo yalitolewa kwa kampuni za watu walio na ushawishi, alisema kila mtu ana haki ya kufanya biashara na serikali.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles