23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia mgeni rasmi tamasha la Utamaduni

Na Clara Matimo, Mwanza

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la utamaduni wa Mtanzania litakalofanyika Septemba 7 na 8, mwaka huu katika Uwanja wa Msalaba mwekundu Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza karibu na makumbusho ya mila na desturi za kabila la wasukuma Bujora.

Tamasha hilo ambalo  limeandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania limelenga kudumisha, kuendeleza, kufundisha na kurithisha utamaduni wa Tanzania kwa vizazi vya sasa ili viudumishe.

Hayo yameelezwa jijini Mwanza na Mratibu wa Tamasha hilo, Chifu Aron Mikomangwa Nyamilonda wa lll, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yatakayoongelewa siku hizo mbili na lengo la tamasha.

Amesema  baadhi ya  mambo yatakayofanyika ni pamoja na michezo ya jadi ikiwemo kurusha mkuki, utakaochezwa na kabila la wamasai, kucheza na fimbo utachezwa na wasukuma bila kusahau mchezo wa bao.

“Tamasha hili litakutanisha machifu kutoka mikoa yote  hapa nchini, kama nilivyosema lengo ni kudumisha, kuendeleza, kufundisha na kurithisha utamaduni wetu kwa watoto wetu hivyo vijana watapata fursa ya kuona na kujifunza jinsi akina mama walivyokuwa wakisaga unga wa kutosha kula familia kwa kutumia mawe au kutwanga kwa kinu maana zamani hakukuwa na mashine za kisasa.

“Watajifunza kuwasha moto bila kutumia kiberiti kama mnavyojua zamani enzi za bibi na babu zetu hakukuwa na kiberiti wazee wetu waliwasha moto kwa kupekecha njiti,” alisema Chifu Mikomangwa ambaye pia ni Katibu Mkuu Usukuma.

Mwenyekiti wa Umoja wa Watemi  wa Usukuma, Itale Charles, amewataka wananchi kuhudhuria kwa wingi  tamasha hilo ambalo litaongelea mambo ya tamaduni, mila na desturi za watanzania ambavyo vyote kwa jumla vinahusisha mahusiano katika jamii  kuanzia ngazi ya  familia.

Kwa upande wake Chifu Edward Makwaiya kutoka Busia Shinyanga,  akizungumzia  utalii wa utamaduni amesema Naamini baada ya  tamasha hili kama nchi tutakuwa na vitu maalum ambavyo vitamvutia mtalii.

“Mtalii anapokuja  baada ya kutembelea mbuga za wanyama anahitaji pia akutane na watu wanaofanya vitu vya tofauti kabisa ambavyo hajawahi kuviona maishani mwake hivyo ndiyo tunasema utalii wa utamaduni, tukiwa navyo kama mtalii alipanga atembelee mbuga za wanyama kwa wiki moja kisha aondoke hakika atavutiwa na atakaa zaidi, imani yangu kwamba tamasha hili litakuwa na matokeo chanya kwa taifa letu,” amesema Chifu Makwaiya na kuongeza:

“Tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutenga muda wake na kuja kushiriki na sisi kwenye tamasha hili pamoja na kujukumu mengi aliyonayo, hii inadhihirisha wazi kwamba lengo lake ni kudumisha, kuendeleza na kurithisha vizazi vyetu utamaduni wetu kama ambavyo wenzetu kabila la wamasai na  wenzetu wa Tanzania Visiwani  Zanzibar wanavyoendeleza tamaduni zao, tunahitaji nchi nzima tuzipe kipaumbele tamaduni zetu,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles