Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka askari wa usalama barabarani kujenga urafiki na watu wanaofanya nao kazi kuliko kuwa kero kwao ili kukabiliana na ajali.
Akizungumza leo Novemba 23, 2021 wakati akizindua maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, yanayofanyika mkoani Arusha, Rais Samia amesema askari wawe msaada ili wananchi wakiwaona wawakimbilie.
“Suala la kusimamia usalama barabarani ni jukumu la Jeshi la Polisi lakini nao sio Malaika, askari wetu wawe na msaada kwa wananchi na sio kero kwa wananchi, wananchi wakiwaona wawakimbilie na sio wawakimbie.
“Kwa sababu ajali nyingine zinatokana na hawa vijana wetu wenye pikipiki, akiona unifomu ziko pale anakata kichochoro, huko anakoenda hajui kuna nini, ajali zinatokea, kwa hiyo askari mjitahidi sana kuwa wenyewe wa usalama barabarani.
“Lakini pia kuna kero ndogongogo zinazolalamikiwa kwa askari wetu kwa mfano suala la kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu au kulazimisha madereva kulipa faini hapo hapo wakati sheria inampa muda dereva kwenda kulipa faini lakini wanang’ana ilipwe hapo hapo unajiuliza kuna nini.
“Jingine ni kwamba kuna ukamataji mwingi wa vyombo, ukipita vituo vya polisi kuna pikipiki nyingi zimepangwa na nyingine haizonekanani kama zimekamatwa jana na leo na utajiuliza kwa nini hizi pikipiki haiondoki pale.
“Kwa sababu kama ni ushahidi wa makosa, makosa yasikilizwe kesi imalizike, hakumumiwe mkosa alafu kazi iendelee.
“Lakini vyombo vinabaki muda na muda, vingine unahisi kama vimetelekezwa na wenyewe, nadhani inagaliwe kwa undani kero hizi ndogondogo zinasababishwa na nini,” ameeleza Rais Samia.
Aidha amesema takwimu zinaonyesha kuwa waendesha pikipiki maarufu bodaboda bado wamekuwa kinara wa kusababisha ajali ambapo kwa miaka mitano wapanda bodaboda 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani, huku majeruhi wakiwa 4,202.
“Hii ni kusema kwamba kwa mwaka mmoja ndani ya kipindi hiki , tumepoteza vijana 445, waendesha bodaboda peke yao na Mahospitali yetu yalikuwa na vijana 850 kila mwaka wanaotokana na ajali za bodaboda au wao kugonga wengine au kusababisha gari liue kwa sababu yao.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania mnaondesha bodaboda, kuwa kinara katika takwimu hizi si sifa njema, niombe sana Jeshi la Polisi mnapoendesha elimu ya usalama barabarani mara nyingi bakini na watu wa bodaboda,” amesema Rais Samia.
Amewataja wengine waliochangia ajali katika kipindi cha miezi ni madereva wa magari binafsi.
Kutokana na hali hiyo, Rais amelitaka Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani kuzidi kutoa elimu kwa vijana waendesha bodaboda.
Aidha amelitaka jeshi hilo kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu hiyo, pamoja na kuwekeza katika utafiti ili kupata suluhisho la kisayansi la kupunguza ajali.