Sheila Katikula na Clara Matimo-Mwanza
Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) kutowabambikizia wananchi bili za maji kwani hali hiyo inasababisha wateja kutumia mbinu mbaya za kuiba maji na kuikosesha Serikali mapato.
Amesema kitendo hicho kinasababisha wananchi kutonufaika na matunda ya kodi zao ambazo Serikali inazitumia kutekeleza miradi mbalimbali ili kuwatatulia changamoto zinazowakabili.
Rais Samia ametoa onyo hilo wilayani Misungwi mkoani Mwanza jana Juni 14, baada ya kuzindua mradi mkubwa wa maji uliojengwa Kijiji cha Nyahiti Kata ya Igokelo ambao uliogharimu Sh bilioni 13.77.
“Mpeni mtu kiwango alichotumia alipe kihalali mkiwabambikizia bili za maji wateja wanakimbia kulipa nao wanatafuta mbinu zao za kutumia maji bila kulipa hivyo kuikosesha Serikali mapato.
“Lakini niwaombe mamlaka zote za maji na wananchi kulipa bili za maji tambueni kwamba fedha tulizozitumia kujenga mradi huu tumekopa ingawa ni mkopo wa riba nafuu lakini tunatakiwa kurudisha, mtakapolipa bili na tozo kwa wakati na ambazo ni halali tutaweza kurudisha mkopo huu na kukopeshwa tena ili tuendelee kujenga miradi mingine yenye tija kwa taifa na wananchi wake,”alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya maji, Mhandisi, Antony Sanga, amesema mradi huo utaongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 42 hadi asilimia 83 katika Wilaya ya Misungwi .
Mhandisi Sanga alisema mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita milioni 4.5 za maji kwa siku ambazo zitatosheleza mahitaji ya wakazi wa Wilaya ya Misungwi ambao mahitaji yao ni lita milioni 3.9 kwa siku.
“Mradi huu umepewa nafasi ya kuongeza uzalishaji kwa baadae kwa kadri mahitaji yanavyoongezeka utaweza kuzalisha zaidi ya lita milioni 6 kwa siku lakini kwa sasa utawahudumia jumla ya wakazi 64,000,”amesema Sanga.
Naye Waziri wa Maji, Juma Aweso, amesema wizara yake haitakuwa kikwazo kwa watanzania kupata maji safi na salama na kwamba mahitaji ya maji katika jiji la Mwanza ni lita milioni 54 uzalishaji wa sasa ni lita milioni 90.
“Mheshimiwa Rais nakumbuka uliponiapisha uliniita ukaniambia nikikuzingua tunazinguana naomba nikuhakikishie mimi na watendaji wa Wizara ya maji ulionipa dhamana kuisimamia hatutakuangusha kwa sababu hatuko tayari kukuzingua.
“Wizara tunaenelea kufanya mageuzi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji tunatambua lengo leko ni kumtua mama wa kitanzania ndoo kichwani na sisi kama wizara tumeanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha nia yako ya dhati kwa wananchi inatimia,”alisema Aweso.
Mradi huo umegharimikiwa na Serikali ya Tanzania, Benki ya uwekezaji ya Ulaya (EIB), Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (Mwauwasa).