32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia ageukia vyombo vya haki nchini

*Asema utawala bora ni muhimu

*Aunda Kamati ya watu 12 kumshauri njia bora ya kuleta matokeo…

Na Mwanadishi Wetu, Mtanzania Digital

RAIS Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati ya Watu 12 wakiongozwa na Jaji Mkuu mstafu Othman Chande na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue kwa lengo la kumshauri njia bora ya kuleta matokeo kwenye vyombo vya haki nchini.

Rais Samia amebainisha hayo leo Jumatano Julai 20, 2022 Ikulu jijini Dodoma wakati akiwaapisha wateule wapya akiwamo Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillius Wambura, ambapo amesema kuwa atafanya mabadiliko zaidi kwenye vyombo vya usalama, ili kuboresha mifumo ya taasisi za kijamii.

“Niseme tu kwamba kwa kifupi Serikali sasa tunakuja na jicho lingine ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo hivi vitakuwa vinanishauri kila mara ili kuwa na jeshi imara la kuijenga Tanzania. IGP (Wambura) tutazungumza baadae,” amesema Rais Samia.

Amefafanua kuwa utawala bora ni muhimu huku akiainisha taasisi hizo.

“Utawala bora ni muhimu, nimeamua kufanya maboresho kwenye mifumo ya taasisi za kijamii, nimeanza na Polisi, Ofisi ya Mashtaka lazima pafanyiwe marekebisho, Takukuru, Magereza, Mamalaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kote tutapita na kufanya marekebisho.

“Tutatazama miundo ya taasisi je inasaidia, inakwenda na yaliyopo duniani, mifumo ya ajira, mafunzo, maadili na nidhamu, lazima tukatazame haya Haki na za watu na kazi na nchi lazima tutazipa kipaumbele,” amesema Rais Samia.

Amebainisha kuwa jambo jingine atakaloliangalia ni mifumo ya utendaji kazi kuona iwapo inafanya kazi kama inavyotakiwa au kuna mazoea yaliyopitiliza na kazi zinafanyika ilimradi tu.

Rais Samia amesema kuwa: “Kuna taasisi zinachukua hatua lawama zinaletwa kwa Rais tumeonewa lakini ukifuatilia unaona walichelewa kumfukuza,” ammesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kuwa kingine kitakachoangaliwa ni mifumo ya upandishaji vyeo ndani ya taasisi za majeshi nchini.

“Upandishaji vyeo kwenye majeshi upoje, getini Ikulu nikitoka natizama wale wanajeshi, nimetizama Dar na hapa Dodoma, mtu anakaribia kustaafu ana miaka zaidi ya 50 hana kitu chochote begani, bega lipo halina kitu ‘flati’, bega linafanana na koplo hii sio sawa,” amesema Rais Samia.

Amefafanua kuwa ameamua kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha kwenye bajeti za majeshilengo likiwa ni kuboresha hali za askari na kumtaka IGP mpya Wambura kwenda kusimamia stahiki za askari.

“Pia sifa za watenda kazi zipoje? …nilikuwa namtania Sirro (IGP aliyeteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe) kwenye jeshi unasikia walianza 300 wakapatikana 200 wengine wameshindwa, huku kwenye Polisi vipi mamabo yakoje?,” amehoji Rais Samia na kuongeza:

“Tukatizame kuna bandia ‘feki’ nyingi wote wanamaliza wanapatiwa kazi, ndio maana kuna mambo ambayo sio ya kimaadili yanafanyika, kwa majeshi yote tutaangalia.

“Huko mbele tunapokwenda tutachujana vizuri ili kujenga majeshi yenye sifa,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemshukuru IGP Mstaafu Simon Sirro kwa utendaji wake huku akisitiza kuwa mabadiliko katika dunia hii hayaepukiki.

“Nianze na shukrani za dhati kwa IGP Sirro, umelitumikia Jeshi la Polisi kwa muda wote, umefanya Mungu alipokujalia, umelisogeza Jeshi la Polisi, lakini jinsi dunia inavyokwenda mabadiliko lazima.

“Nimpongeze IGP Wambura, nachotegemea kutoka kwako ni kuona mabadiliko makubwa na ufanisi ndani ya Jeshi la Polisi, usalama wa raia na mali zao unaimarika ndani ya Jeshi la Polisi,” amesema Rais Samia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles