BAADHI ya vigogo wa Serikali ya Afrika Kusini ‘walijichotea’ mamilioni ya fedha kupitia mkataba wenye thamani ya Randi milioni 150 (zaidi ya sh bil. 23 za Tanzania) walioingia Wizara ya Afya na kampuni ya Digital Vibes.
Hayo yamefichuliwa na uchunguzi wa Tume Maalumu ya Rais Cyril Ramaphosa, ambapo kiongozi huyo aliwasilishiwa ripoti mwanzoni mwa Julai, mwaka huu, kabla ya kubariki ianikwe na kuufikia umma.
Kupitia ripotin hiyo, uchunguzi unaonesha kampuni hiyo ya habari ya Digital Vibes iliwapa rushwa vigogo wa Wizara ya Afya, kabla ya kupewa zabuni ya kuendesha shughuli za Bima na taarifa zihusianazo na janga la Corona.
Kabla ya Rais Ramaphosa kukabidhiwa ripoti miezi miwili iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Afya, Zweli Mkhize, alijiuzulu na inafahamika kuwa ana ukaribu mkubwa na wamiliki wa kampuni hiyo ya Digital Vibes, Tahera Mather na Naadhira Mitha.
Ikifafanua upigaji uliojitokeza, ripoti inaonesha Digital Vibes walimpa Mkhize kiasi cha Randi 6,720, Randi 300,000 alipewa mtoto wake wa kiume, Dedani Mkhize, ambaye pia alinunuliwa gari aina ya Land Cruiser lililogharimu Randi 160,000. Katika skendo hiyo, amewatajwa pia vigogo wa Kamati ya Tathimini ya Zabuni (TEC), akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano, Popo Maja.