32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Namibia apata Tuzo ya Mo Ibrahim

POHAMBAMwandishi Wetu na Mashirika ya Habari
RAIS anayemaliza muda wake nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba, ameshinda tuzo ya Mo Ibrahim inayotolewa kwa kiongozi wa Afrika aliyeonyesha uongozi bora.
Tuzo hiyo yenye thamani ya dola za Marekani milioni tano (sawa na Sh bilioni 9.2 za Tanzania) ni kubwa zaidi duniani kutolewa kwa mtu mmoja mmoja.
Fedha hizo hutolewa kila mwaka kwa kiongozi wa kuchaguliwa aliyetawala vizuri kwa kuinua viwango vya maisha ya raia wake na kisha kuondoka madarakani kwa amani.
Lakini mwaka jana tuzo hiyo ilikuwa ya nne kwa kipindi cha miaka mitano kukosa mshindi.
Pohamba, mpiganaji wa zamani wa waasi aliyepigania uhuru wa nchi yake, alitumikia mihula miwili kama rais wa Namibia.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, na mara nyingine mwaka 2009. Nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Rais mteule, Hage Geingob.
Pohamba alikuwa mwanachama mwanzilishi wa South West Africa People’s Organisation (SWAPO), vuguvugu la msituni lililoendesha harakati za miongo mingi ya kupigania uhuru dhidi ya Afrika Kusini.
Tangu ipate uhuru mwaka 1990, SWAPO imetawala siasa za nchi hiyo ikishinda kwa wingi wa kura katika uchaguzi. Mo Ibrahim ni Mwingereza mwenye asili ya Sudan, mhisani na mfanyabiashara wa sekta ya mawasiliano ambaye alijitengenezea mabilioni ya fedha kwa kuwekeza Afrika.
Alizindua tuzo hiyo ili kutoa msukumo kwa viongozi wa Afrika kuondoka madarakani kwa amani.
Tuzo ya kwanza ilitolewa mwaka 2007, ikienda kwa Rais wa zamani wa Msumbiji, Joaquim Chissano, ambaye tangu hapo amekuwa msuluhishi katika migogoro kadhaa barani Afrika.
Mo Ibrahim hutoa dola milioni tano kwa kipindi cha miaka 10 na dola 200,000 kila mwaka kipindi chote kilichobakia cha kiongozi husika.
Pohamba anakuwa mshindi wa kwanza wa tuzo hiyo tangu ichukuliwe mara ya mwisho na Rais wa zamani wa Cape Verde, Pedro De Verona Rodrigues Pires mwaka 2011.
Alipoulizwa kwanini ni viongozi wachache wameshinda tuzo hiyo tangu izinduliwe, Ibrahim alisema taasisi yake haiwezi kutoa tuzo kwa marais wanaopata viwango vya chini.
“Nadhani Pohamba ametuonyesha mfano nzuri wa aina yake wa kiongozi ambaye ameingia madarakani kidemokrasia na kuhakikisha nchi yake imeboresha elimu, ustawi na mchangamo wa kijamii.
“Ni tuzo kwa uongozi mzuri na hivyo hatuwezi kuitoa kwa wanaopata viwango vya chini.
“Iwapo tuzo hii itatolewa kwa viongozi wa Ulaya, je, wadhani ni wangapi wangeshinda tuzo hii kipindi cha miaka nane tangu ianzishwe?” alisema na kuhoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles