29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Msengi Kusikiliza kesi ya Wakili Mwale

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

KESI ya utakatishaji fedha haramu inayomkabili wakili maarufu jijini Arusha, Medium Mwale na wenzake watatu, imeanza kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mbele ya Jaji Fatuma Masengi.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwishoni mwa wiki baada ya Jamhuri kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya, kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali ya mashtaka 42 yanayowakabili.
Tibabyekomya alidai washtakiwa wote walikubali majina yao kuwa Median Mwale, Don Bosco Gichana, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi.
Alidai washtakiwa walikana maelezo mengine yote waliyosomewa mahakamani hapo.
Inadaiwa kati ya mwaka 2008 na 2010, mshtakiwa Mwale aliwasilisha nyaraka za uongo za marejesho ya kodi nchini Marekani.
Inadaiwa nyaraka hizo zilizokuwa na anuani ya waliokula njama pamoja Marekani, zilikuwa na taarifa za uongo kuhusu kumbukumbu za wafanyakazi na madai ya kodi.
Nyaraka hizo zilikuwa na hundi zenye thamani ya dola za Marekani 5,296,327.25 ambazo aliziwasilisha kwa kutumia jina la John Adams, hundi yake ilikuwa ya dola za Marekani 200,790.56, Nyambao Hollo (Dola 731,889), Mosoti Haye (Dola 275,428), Syron Hess(Dola 200,790.56), Joshua Husbo(Dola 104,408) na Dale Houston (Dola 55,386.35) .
Nyingine ni Magara Nolan (Dola 327,188), Delvin Fields (Dola 924,126), Clarence Sample (Dola 54,122.81), Edga Johnson (Dola 355,964), Herbert Breneman (Dola 521,824), Curtis Ciobb (Dola 597,731), Jefferey Glaysbrook (Dola 204,134), Brian Kirksey (Dola 6,226.60) na Omwamba Cannon ( Dola 527,308).
Hundi hizo zote zinadaiwa kuwa zilikuwa zinasimamiwa na mshtakiwa Mwale ambaye kwa kula njama na washtakiwa wenzake, alizihamisha na kwenda kulipwa benki na CRDB Arusha kati ya mwaka 2009 na 2011.
Mshtakiwa kwa kuitumia kadi ya makazi ya kughushi anadaiwa kuwa aliwawezesha Ogembo Chacha na Gregg Mwita kufungua akaunti CRDB na Desemba 18 mwaka 2009 hundi mbili za marejesho ya kodi kutoka Marekani zenye thamani ya dola za Marekani 95,836 na 76,536 zililipwa kwa Gregg kama marejesho ya kodi.
Wakili wa Serikali alidai hundi za uongo za marejesho ya kodi kutoka Marekani zilikuwa 15 na zililipwa kupitia akaunti ya Moyale Precious Gems and Minerals Enterprises jumla ya dola za Marekani 5,123,624.84 ambazo zilitolewa na kuhamishiwa katika akaunti ya mshtakiwa wa kwanza namba 3300195969 iliyopo Benki ya KCB Tanzania Ltd Arusha na akaunti namba 009-243050-002 kwa jina la Noman Mahaboub Muhamad Al-Agbary iliyopo Yemen na akaunti nyingine kwa jina la Salim Ally iliyopo Uingereza.
“Agosti 4 mwaka 2011, katika upekuzi, mshtakiwa wa kwanza akiwa chini ya ulinzi wa polisi alitumia fedha hizo za Marekani kununua mali mbalimbali ikiwamo shamba katika Kijiji cha Ekenywa Arumeru mkoani Arusha, gari aina ya BMW T 907 BTS, gari aina ya Landrover Discovery T 643 BTS.
“Nyumba mbili, moja yenye thamani ya dola za Marekani 80,000, alinunua nyumba nyingine iliyopo kiwanja namba 22 kilichopo Ilkiurei Arumeru na nyumba namba 21 eneo la Njiro jijini Arusha,” ilidaiwa katika maelezo ya awali.
Washtakiwa walikana maelezo yote hayo, na kesi iliahirishwa hadi tarehe nyingine ambayo mahakama itapanga kwa ajili kuendelea kuisikiliza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles